Na Mashaka Mgeta, MWANZA
ILIANZA kama ‘kumkimbiza mwizi kimya-kimya’, ikaziondoa hatua kwa hatua timu ilizokutana nazo kabla ya kuingia fainali iliyochezwa leo.
Ni timu iliyokuwa na ‘utitiri’ wa rasilimali zilizotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, ikipata motisha kwa kutembelewa na Katibu Tawala Mkoa, Rashid Mchatta na kupokea salaam za moja kwa moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian.
Habari za ubora wa uvutaji kamba wake zikaenea katika pande zote za jijini Mwanza, walio wengi miongoni mwa wanamichezo wakazidi kuitaja, kuisifu na kuitamani timu ya Wavuta Kamba Wanawake wa Sekretarieti ya Mkoa (RS) ya Mkoa huo.
Leo Septemba 16, 2025, mchana kweupe, timu hiyo ikakutana na wavuta kamba mahiri wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili kumpata mbabe atakayetwaa taji la Ubingwa wa SHIMIWI 2025.
RS Tanga inayoongozwa na Nahodha ambaye pia ni ‘Stoper’ wake, Ruth Jacob, ikaingia uwanjani kuwakabili TAKUKURU, ambapo ‘haikuchukua muda’, mashabiki lukuki walioujaza Uwanja wa CCM Kirumba, wakapaza sauti zao wakiimba kwa kurudiarudia, ‘RS Tanga yeeeeeeeee,….wengine wanaitikia ‘yeeeeeeee.’
Kwa upande wao, wachezaji wa michezo mingine kutokea RS Tanga nao hawakupoa, wakiongozwa na Mchezaji Mhamasishaji, Erimina Kinabo.
Hatimaye kwa ushindi dhidi ya TAKUKURU, RS Tanga ikaipeleka furaha kwa wakazi wa Mkoa huo wenye kauli mbiu ya ‘Lango Kuu la Uchumi Afrika Mashariki.’
RS Tanga, itaondoka jijini Mwanza kesho alfajiri kurejea nyumbani, ambapo Katibu Tawala Msaidizi (Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu), Sebastian Masanja, amesema wakazi wa mkoa huo wameandaa mapokezi ya ‘kukata na shoka’; huku Mhe Balozi Dkt Batilda akiwaandalia hafla ya kuwapongeza.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.