CCM TANGA YASEMA, KWA MAKONDA ZEGE HALILALI
Na Mashaka Mgeta, TANGA
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Selemani Sankwa, amesema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Paul Makonda, atatumia falsafa ya ‘zege halilali’ kutatua kero sugu zinazowakabili wananchi katika ziara yake inayoanza hii Jumamosi mkoani humu.
Ndugu Sankwa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake leo Ijumaa ya Januari 19, 2024, kutoa taarifa ya ziara ya Ndugu Makonda itakayoanza Januari 20 hadi 22, mwaka huu.
‘’Miongoni mwa malengo ya ziara hii ni kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo atakayopita na wale watakaotoka sehemu nyingine kuja kuhudhuria mikutano yake…utatuzi huo unafanyika kwa falsafa ya zege halilali, yaani kila kero inapatiwa ufumbuzi hapo hapo,’’ amesema huku akihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi.
Kwa mujibu wa Sankwa, malengo mengine ya ziara hiyo itakayoanzia Mkata wilayani Handeni, Pangani, Tanga Mjini, Muheza, Handeni na kumalizikia Korogwe, ni kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, miradi ya maendeleo na uhai wa chama hicho kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji baadaye mwaka huu.
Sankwa amesema katika ziara hiyo, Ndugu Makonda atakagua ujenzi wa daraja la Mto Pangani kisha kufanya mikutano ya hadhara jijini Tanga, Muheza, Segera na kumalizia Korogwe.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.