Na Mashaka Mgeta, LUSHOTO
IPO dhana iliyojengeka na kugeuzwa kuwa sababu ya kushindwa kutekelezwa kwa baadhi ya miradi ya maendeleo inayogharamiwa na Serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, sababu ikitajwa ni kuwa pembezoni mwa nchi.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Mhe Zephania Sumaye, anajenga hoja iliyo kinyume na dhana hiyo, na kubainisha uwezekano wa kutekeleza miradi husika kwa ufanisi kwenye maeneo hayo kwa ufanisi na mafanikio.
Mhe Sumaye anasema, baadhi ya maeneo ya wilaya ya Lushoto yapo pembezoni, lakini ipo miradi mingi iliyotekelezwa kwa ufanisi, sababu kuu zikiwa ni nidhamu ya matumizi ya fedha, uadilifu na ufuatiliaji wa karibu.
Miradi mitatu ya Shule ya Amali ya Shita, kata ya Magamba, madarasa mawili ya Shule ya Awali ya Shule ya Msingi Mabughai na bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kwalei, imetembelewa na Kamati ya Siasa ya Mkoa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuridhishwa na ubora unaolingana na thamani yake.
Miradi hiyo ipo kwenye maeneo yaliyo nje ya Makao Makuu ya Wilaya ya Lushoto, ambapo Mhe Sumaye anasema, umbali wa kijiografia na uduni wa miundombinu hasa barabara kwa baadhi ya maeneo, havikuwa sababu ya kukwama kwa miradi hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, Baraka Michael, pamoja na mambo mengine, amesema, bweni la Shule ya Sekondari ya Kwalei lenye uwezo wa kuchukua wanafunzo 80, limegharimu jumla ya Shilingi milioni 85.
Amesema hatua ya kuishirikisha jamii tangu kupokea fedha za mradi huo na mchakato wa ujenzi wake, viliongeza nguvu ya wananchi kuchangia ujenzi na kulinda miundombinu yake isiharibiwe.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi wa hiyo, Mohamed Amir amehimiza ushirikiano wao (wazazi), walimu na jamii, kuwalinda wanafunzi wa shule hiyo ili wasome kwa amani, salama na kufikia nia na ndoto zao kwa maslahi ya taifa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwalei, Silas Charles, amesema wamejipanga kwa ulinzi wa wanafunzi, na kwamba yeyote atayehusika kudhulumu haki zao, atachukuliwa hatua kali za kisheria kuwa fundisho kwa jamii.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.