Karibu mgeni Mwenge, mkoani kwetu Tanga,
Na wenyeji tukuchunge, kwa bashasha na kuringa,
Mwakidila hadi Kange, wa Duga na Gongagonga,
Karibu mgeni Mwenge, Tanga tunakusubiri.
Nuru yako yaangaza, mema kuyapigania,
Unaliondoa giza, hapa kwetu Tanzania,
Daima unatukuza, haki na demokrasia,
Karibu mgeni Mwenge, Tanga tunakusubiri.
Unamulika uovu, ndani na nje ya nchi,
Unakemea uvivu, uwatoke wananchi,
Wahimiza ushupavu, mfananowe wa ‘winchi’,
Karibu mgeni Mwenge, Tanga tunakusubiri.
Waleta matumaini, pasipo matumaini,
Unahimiza amani, iwe kwetu tamaduni,
Maendeleo mikoani, wakagua kwa yakini,
Karibu mgeni Mwenge, Tanga tunakusubiri.
Unaziondoa chuki, kiburi hata dharau,
Umoja kuumiliki, kutimiza yetu kiu,
Vurugu kwenye handaki, hayo tumeyasahau,
Karibu mgeni Mwenge, Tanga tunakusubiri.
Miradi kwa bilioni, fedha zilizotolewa,
Hazifichwi mifukoni, hadharani kuwekewa,
Mijini na vijijini, kote zimepokelewa,
Karibu mgeni Mwenge, Tanga tunakusubiri.
Njoo ukaikague, miradi ilo’tulia,
Salaam zimfikie, fedha alotuletea,
Tunatamba na tunaye, ni wetu Mama Samia,
Karibu mgeni Mwenge, Tanga tunakusubiri.
Shairi hili limeandaliwa na:-
Mashaka B. Mgeta,
Afisa Mawasiliano Serikalini,
RS - Tanga
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.