Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
TAASISI zinazohusika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikihusisha inayotembelewa, kukaguliwa, kuwekewa mawe ya msingi ama kufunguliwa na Mwenge wa Uhuru, zimetakiwa kuwa na mikakati ya utunzaji endelevu wa miradi hiyo.
Rai hiyo imetolewa jana Mei 28, 2025 na Katibu Tawala Msaidizi (Utawala na Rasilimali Watu) wa Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga, Sebastian Masanja, alipokagua maandalizi ya miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru 2025 wilayani Handeni. Mwenge wa Uhuru 2025 utawasili mkoani humo Juni 6 na kukimbizwa kwenye Halmashauri 11 hadi Juni 17, 2025 utakapopelekwa Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Masanja aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amesema uimara na maelekezo ya Mwenge wa Uhuru kwa hatua tofauti za miradi ya maendeleo, vinapaswa kuwa sehemu ya desturi za kawaida za utekelezaji na uendelezaji wa miradi hata Mwenge huo unapopita.
”Mwenge wa Uhuru ambao mwaka huu una ujumbe unaosema, ”Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu” uwe kichocheo kwetu kuwa ni mipango ya utekelezaji na utunzaji endelevu wa miradi ya maendeleo,” amesema.
Ameyasema hayo alipokuwa akikagua ujenzi wa nyumba moja yenye uwezo wa kutumiwa na familia mbili katika Shule ya Sekondari Kabuku Ndani, inayogharimu Shilingi milioni 98.
Mbali na mradi huo, Masanja alitembelea na kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi katika Shule ya Msingi Kabuku Mjini yenye thamani ya Shilingi milioni 36.3 ambapo Shilingi milioni 11.3 zimetokana na serikali ya kijiji, michango na nguvu za wananchi wakati Shilingi milioni 25 zimetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Pia, Masanja alikagua ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika zahanati ya Msasa lenye thamani ya Shilingi milioni 102.2 zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mji Handeni, Mfuko wa Jimbo na nguvu za wananchi.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.