Na Mwandishi Wetu, HANDENI
MKUU wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Mhe Albert Msando, amesema utendaji kazi wa viongozi katika kuwatumikia wananchi, unapata ufanisi zaidi kwa kuishirikisha tasnia ya habari, ili kuwezesha taarifa sahihi na za kweli kuifikia jamii kwa weledi.
Mhe Msando aliyasema hayo jana Februari 5, 2025 alipokutana ofisini kwake na ujumbe wa Klabu ya Waandishi wa Habari T(TPC), chini ya Mwenyekiti , Lulu George, Makamu Mwenyekiti, Burhan Yakub na Idd Hassan (Mratibu).
Pia walikuwepo Afisa Mawasiliano Serikalini - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mashaka Mgeta na Mwandishi wa Habari wa ITV, Kassim Sonyo.
Mhe Msando amesema, ushirikiano mwema na wadau wa maendeleo vikiwemo vyombo vya habari, ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambayo yeye anayasimamia kwa ufasaha wilayani humo.
Amesema waandishi wa habari wapo huru kufanya kazi zao wilayani Handeni, angalizo pekee likiwa ni kutokiuka sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Kwa upande wake, Lulu alisema ziara hiyo ni mpango wa TPC kuimarisha mahusiano na ushirikiano mwema kati ya tasnia hiyo na wadau wa habari mkoani humo.
Alisema, taasisi za habari zinatambua umuhimu wa kuimarisha mahusiano na ushirikiano kwa wadau, na utekelezaji wa majukumu ya wanahabari kwa weledi na kufuata sheria zinazohuziana na tasnia hiyo.
Kassim Sonyo alisema, pamoja na uwepo wa matakwa ya sheria, ipo haja ya kuchochea mahusiano mema kati ya wanahabari na wadau wa sekta hiyo ikiwemo Serikali, ili kufikia malengo yenye tija kwa maendeleo na ustawi wa watu.
Naye Mgeta alisema, mpango wa TPC kukutana na wadau wa habari wakiwemo viongozi wa Serikalini mkoani Tanga, utachangia kuboresha na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya pande mbili hizo.
Amesema, Mkuu wa Mkoa huo, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, anatambua umuhimu wa wanahabari katika kutangaza maendeleo yaliyofikiwa na Serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, na hivyo kuweka msisitizo wa kuimarisha mahusiano mema kati ya pande zote.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.