Na Emma Kigombe, OMM TANGA
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, imetoa rai kwa jamii kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya mtoto kwenye maeneo yao.
Amesema, malezi na makuzi ya mtoto wa umri wa kuanzia mwaka 0 hadi minane, ni sehemu ya vipaumbele vya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kupitia Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM).
Program hiyo inalenga kuimarisha afya, lishe, malezi yenye mwitikio, ulinzi na fursa za ujifunzaji wa awali kwa mtoto wa Tanzania.
Leo Julai 9 2025, Mchatta ameongoza kikao kazi cha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa PJT-MMMAM, kilichowakutanisha wajumbe wa kamati za MMMAM kutoka halmashauri 11 za mkoa huo.
“Misemo ya wahenga kama vile ‘samaki mkunje angali mbichi’ na ‘mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’ inatufundisha kwamba msingi wa maisha ya mtoto hujengwa katika umri mdogo. Ni wajibu wetu sote kuwekeza nguvu na rasilimali katika hatua hii muhimu ya maisha ya mtoto,” amesema Mchatta.
Takwimu za Utafiti wa Viashiria vya Afya (TDHS) wa mwaka 2022 zinaonesha kuwa, asilimia 47.4 ya watoto nchini wanakua kwa viwango stahiki, huku Tanga ikiwa na asilimia 46.6.
Mchatta amesema takwimu hizo ni ishara kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya, kuhakikisha watoto wote wanapata mazingira bora ya makuzi na maendeleo ya mwili, akili na hisia.
Aidha, amesema changamoto kama watoto wa mitaani, udumavu, utumikishwaji, ukatili, maradhi na ufaulu mdogo wa watoto, vinachangiwa na upungufu kwenye malezi ya awali.“Hivyo ni muhimu kwa familia, jamii na Serikali katika ngazi zote kushirikiana kikamilifu kutekeleza afua za MMMAM, “ amesema.
Mchatta, amezitaka halmashauri za mkoani humo, kutenga na kutumia rasilimali (hata kama ni kidogo) kwa ajili ya watoto.Kikao hicho kinatarajiwa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa afua za MMMAM, kubadilishana uzoefu, na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha utekelezaji wake kwa mustakabali bora wa watoto wa Mkoa wa Tanga.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.