Na Mashaka Mgeta, MOROGORO
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas, amewataka Maafisa Mawasiliano na Habari wa Serikali, kuweka na kutumia mikakati ya mawasiliano kutoa taarifa sahihi na kushughulikia matukio yanayohusiana na majanga yanayotokea kwenye maeneo yao.
Dk Abbas alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali kati ya Agosti 11, 2017 hadi Januari 31, 2020 alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Februari 14, 2023 alihamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii akiwa katika wadhifa huo hadi sasa.
Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) ulioanza Aprili 8 na kufikia ukomo wake Aprili 12, 2025 mjini Morogoro.
Dk Abass amesema yapo mambo yanayotarajiwa na yasiyotarajiwa kutokea kwenye taasisi za umma, yakiwa ni dharura ama majanga, hivyo ni jukumu la Maafisa hao kuyabaini mapema na kuushauri uongozi namna bora ya kukabiliana nayo.
Amesema, majanga yanapotokea yanawagusa Maafisa Mawasiliano na Habari wa Serikali, hivyo kuwajibika kwa kuwa na mkakati wa kuyakabili, kutoa taarifa sahihi na kulinda hadhi ya taasisi zao.
Kwa mujibu wa Dk Abbas, utoaji taarifa sahihi wakati wa majanga unachangia kujenga imani kwa umma, kwamba taasisi husika inatambua, kushughulikia na kuepusha upotofu kuhusu janga husika.
Naye Mwenyekiti wa TAGCO, Karimu Meshack amesema Maafisa Mawasiliano na Habari wanapaswa kutambua uhusika wao wakati wa majanga na kuepuka kasumba ya kujiweka kando kwa visingizio kama vile ‘kutoshirikishwa’,
Naye Mtafiti na Mtaaluma wa Mkakati wa Mawasiliano wa Chuo Kikuu cha dar es Salaam, Dk Sophia Ndibalema amesema kukaa kimya wakati wa majanga, kunatoa mwanya wa wasiokuwa na dhamana, kutoa taarifa zinazoweza kuibua taharuki ama kuipotosha jamii.
Mwisho
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.