DK BITEKO ATOA SIKU 49 UTATUZI CHANGAMOTO ZA WAUGUZI, WAKUNGA
Na Mashaka Mgeta, OMM-TANGA
NAIBU Waziri Mkuu, Mhe Dk Doto Biteko, ameiagiza Wizara ya Afya kutumia siku 49 zilizobaki kufikia ukomo wa mwaka wa fedha 2023/2024, kushughulikia changamoto zinazowakabili wauguzi na wakunga, hususani upandishaji madaraja, kuongoza na kushiriki vikao vya uamuzi kwenye maeneo yao ya kazi.
Mhe Dk Biteko, ametoa maelekezo hayo katika hotuba aliyoitoa kwenye maadhimisho ya Siku ya Uuguzi Duniani iliyofanyika kitaifa jijini Tanga, ambapo pia alifunga rasmi Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 51 wa Chama Cha Wakunga Nchini (TANNA).
Maelekezo ya Mhe Dk Biteko, yametokana na hoja zilizowasilishwa kwa nyakati tofauti na Rais wa TANNA, Alexanda Baluya na Katibu Mkuu wa chama hicho, Samwel Mwangoka kwenye maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na wauguzi na wakunga zaidi ya 2000 kutoka mikoa ya Tanzania Bara.
Viongozi hao waliwasilisha changamoto kadhaa zinazowakabili wauguzi na wakunga, zikiwemo kutopandishwa madaraja pindi wanapotoka kujiendeleza kielimu, na kutoruhusiwa kushika nafasi za uongozi ama kushiriki vikao kwenye vyombo vya maamuzi yanayohusiana na sekta ya afya katika maeneo yao ya kazi.
Kwa mujibu wa viongozi hao wa TANNA, hatua hiyo inawavunja moyo na kujenga dhana kuwa ni kada iliyopo ‘daraja la pili’, licha ya ukweli uliopo kwamba wanahusika kwa asilimia 80 ya utoaji huduma za afya nchini.
Mhe Dk Biteko amesema, wauguzi na wakunga ni kada zinazotegemewa kwa kiasi kikubwa katika uboreshwaji wa huduma za afya nchini, hivyo hoja za upandishwaji madaraja na kupewa fursa za kuongoza ama kushiriki vikao kwenye vyombo vya uamuzi kwenye maeneo yao ya kazi, zinapaswa kupatiwa majawabu ndani ya mwaka huu wa fedha.
Kwa mujibu wa kalenda, mwaka wa fedha wa 2023/2024 unafikia kilele chake Juni 30, 2024 ikiwa ni siku 49 zilizobaki kufikia ukomo wa maelekezo hayo yaliyopokewa kwa shangwe kubwa na washiriki wa kongamano na mkutano huo.
Mhe Dk Biteko amesema, serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya sekta ya afya, hali inayoposwa kuakisiwa kwa ubora wa huduma na mazingira ya kazi kwa watoa huduma za afya wakiwemo wauguzi na wakunga nchini.
‘’Sitaki kuingilia mambo ya kitaaluma, lakini kama kuna kiongozi mzuri kwa nini azuiliwe kuongoza kwa sababu tu ni muuguzi…kwa nini umuondoe kwenye vikao vya uamuzi kwa vile tu ni muuguzi,’’ amehoji Mhe Dk Biteko na kuongeza:-
‘’Kama tatizo lipo kwenye sheria ama kanuni za muundo, basi hilo mlishughulikie haraka. Kazi yangu nikiwa msimamizi wa shughuli za serikali ni kutoa muda ili mambo yaende kwa wakati…na ninaagiza suala hili lishughulikiwe ndani ya mwaka huu wa fedha.’’
Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk Mollel amesema, wizara hiyo inasimamia dhamira ya Mhe Rais Dk Samia kutambua umuhimu wa kada ya wauguzi na wakunga, na kwamba hoja zilizowasilishwa na ambazo ziliwahi kutolewa kwa viongozi wakuu wan chi kwa nyakati tofauti, zimeanza kushughulikiwa.
Dk Mollel amesema, wauguzi na wakunga ni mfano wa ‘jiwe la msingi’ kwenye mkakati na mipango ya uboreshaji wa sekta ya afya nchini, hivyo hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kuhusiana na upandishaji madaraja na uongozi, ili kuiweka dhana hiyo kwenye vitendo na uhalisia wake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amesema uongozi wake unaendelea kufuatilia kwa karibu mazingira bora yanayowahusu wauguzi na wakunga, ili yaakisi uboreshwaji wa sekta ya afya uliofanyika mkoani humu kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu ya Mhe Rais Dk Samia kuwepo madarakani.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, Ustaadhi Rajab Abdulrahaman, ameitaka jamii kutambua kazi kubwa zinazofanywa na wauguzi na wakunga na kwamba, kwa wachache wanaokiuka maadili ya kazi hizo, washughulikiwe kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.