Na Mashaka Mgeta, HANDENI
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Dk Ashatu Kijaji, amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi, ili kufikia azma ya kujitegemea kwa maendeleo na ustawi wao.
Mhe Dk Kijaji amesema kukamilishwa kwa miradi hiyo ni miongoni mwa vipaumbele na maagizo ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa viongozi wa wilaya, halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji zilizo katika ngazi za msingi kwenye jamii, kunapobuniwa, kuibuliwa na kuanzishwa miradi hiyo.
Ameyasema jana Januari 10,2025 katika kijiji cha Kwedikwazu Mashariki wilayani Handeni, kufuatia rai iliyowasilishwa na wakazi wa kijiji hicho wakitaka zahanati iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2013, na kutengewa fedha na halmashauri ya wilaya ya wilaya ya Handeni, ikamilike ifikapo Januari 30, mwaka huu kama ilivyoelezwa na waziri huyo.
Mhe Dk Kijaji anayehitimisha ziara yake ya siku tano mkoani Tanga leo, amesema agizo na nia ya Mhe Rais Dk Samia kuhusu miradi inayoanzishwa kwa nguvu za wananchi ni kukamilisha kwake, hivyo kama ikishindikana kufikia hatua hiyo, inakuwa ni ‘mzigo’ unaopaswa kubebwa na viongozi wa LGAs kwenye maeneo husika.
‘’Mhe DC (Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe Albert Msando), kama zahanati hii haitakamilika ifikapo Januari 30, 2025, hili halitakuwa jambo la Mhe Rais Dk Samia ambaye Septemba 4, 2024, alileta Shilingi milioni 50 kupitia halmashauri ya wilaya Handeni ili kumalizia ujenzi huu…litakuwa jambo lako,’’ amesema.
Hata hivyo, Mhe Msando amesema, usimamizi wa ujenzi wa zanahati hiyo umefanyika kwa vipindi tofauti kupitia ofisi yake, na kwamba uhakika wa kukamilika kabla ama tarehe 30 Januari, 2025 ni wa uhakika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Saitoti Stephen, amesema kukamilisha kwa zahanati hiyo kutawapunguzia wakazi wa Kwedikwazu Mashariki kadhia ya kufuata huduma za afya kwenye kituo cha afya Kabuku, umbali wa takribani kilomita tano.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.