Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
ANAPOONGEA, ukamsikiliza kwa makini huku ukimtazama mwonekano wake, hatua kwa hatua, unapata urahisi wa kugundua na kuamini kwa haraka, usawa uliopo kwa kauli na matendo yake.
Hana hulka ya kuzungumza sana japo ni mcheshi, alijaliwa staha, umakini, utulivu na usahihi wa kila anachokitamka, kikilenga maana anayoikusudia.
Katibu Tawala Mkoa (RAS) wa Tanga, Rashid Mchatta (kulia kwenye picha), amekabidhiwa ofisi leo Juni 30, 2025, ikiwa ni siku ya mwisho wa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Mtangulizi wake, Pili Mnyema, aliyehamishwa kuwa RAS wa Mkoa wa Pwani anapotokea Mchatta, amemkabidhi ofisi hiyo kwenye hafla iliyohudhuriwa na watumishi wa umma, viongozi wa dini, wanasiasa, sekta binafsi walioongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian.
Ilipofika zamu kuzungumza, akiwa ametanguliwa na Mnyema, Mchatta akampongeza mtangulizi wake huyo, kutokana na shuhuda zenye sifa na wasifu uliodhihirisha umahiri wa uongozi wake, alipokuwa RAS wa Tanga kwa kipindi cha takribani miaka minne na nusu.
Mchatta akasema, kauli za watumishi wa umma na wawakilishi wa kada nyingine kumhusu Mnyema, ni ishara kubwa ya mazingira bora, uwezo, weledi na uadilifu wake uliwezesha pia kuimarisha ufanisi, umoja na mshikamano mkoani Tanga.
Akasema, yeye (Mchatta) si mzungumzaji sana, bali katika kutenda na kwamba anataka siku Mungu akijalia akaondoka (Tanga) kwa tukio kama la leo (kuagwa), apate sifa zinazolingana na anazopewa Mnyema.
Mchatta akasema kutokana na hali hiyo, wakazi wa Tanga na viongozi waliopo, wanapaswa kumpima kwa kazi atazozitenda na uwajibikaji wake.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Batilda Burian, amesema uzoefu wa maeneo tofauti aliyofanya kazi, yanatoa uhakika wa mabadiliko yanayotarajiwa kutoka kwa Mchatta.
Miongoni mwa uzoefu huo ni namna bora ya kubuni, kupanga na kutekeleza mkakati wa ukuzaji viwanda mkoani Tanga, kama ilivyokuwa katika Mkoa wa Pwani.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.