Na Emma Kigombe, OMM TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amewataka viongozi na wakuu wa taasisi za Serikali mkoani humo, kujenga na kukuza utamaduni wa maadili na uadilifu mahali pa kazi vikiwa ni sehemu ya msingi wa maendeleo endelevu ya taifa.
Mhe Balozi Dkt Batilda, ameyasema hayo leo Juni 25, 2025 jijini Tanga, wakati akifungua mafunzo ya Maadili na Utawala Bora kwa Viongozi Wakuu wa Taasisi za Serikali, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushirikiana na Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA).
Amesema utawala bora na uadilifu ni nguzo muhimu za maendeleo, na kwamba viongozi wa taasisi ndio vinara wakuu wa kuyaendeleza na kuyasimamia maadili hayo.
Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, baada ya mafunzo hayo, Serikali itafuatilia kwa karibu kubaini ikiwa kuna mabadiliko chanya ya kimaadili na kiutendaji katika taasisi hizo.
Mkuu wa Mkoa huyo ametoa wito kwa taasisi zote kuhakikisha kuwa wasaidizi wa viongozi wakuu pia wanapatiwa nafasi ya kushiriki mafunzo hayo, ili kukuza uelewa wa pamoja kuhusu maadili na uwajibikaji.
Amesema, Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameweka nguvu kubwa katika eneo la utawala bora na maadili, na ndio maana mara kwa mara huchukua hatua za maboresho kuhakikisha dhana hiyo inatekelezwa ipasavyo katika taasisi zote za umma.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanawashirikisha viongozi wakuu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano wa kitaifa katika kukuza maadili, uwajibikaji na utawala bora nchini.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.