Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
ATHARI zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuwepo kwa wadaiwa sugu, vimebainika kuathiri ukusanyaji mapato wa Mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani Tanga.
Taarifa ya Sekretarieti ya Mkoa (RS) iliyosomwa na Mkuu wa Idara ya Mipango, Amina Said kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) Machi 6, 2025, imeeleza, kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, mvua kubwa iliyonyesha wilayani Muheza, ilipukutisha maua ya machungwa, zao linalochangia takribani asilimia 30 ya mapato yake.
Hali hiyo ilisababisha kushuka kwa uzalishaji, na makusanyo yakawa Shilingi 1,198,907,161 badala ya Shilingi 3,280,710,000, ikiwa ni asilimia 37 kati ya 50 zilizokusudiwa.
Wakati mvua nyingi zikinyesha Muheza, wilaya ya Kilindi ilikabiliwa na ukame kiasi cha kupunguza uzalishaji wa mahindi na maharage yaliyo chanzo kikuu cha mapato yake.
Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ilipangiwa kukusanya Shilingi 3,561,693,000, lakini ikakusanya Shilingi 1,500,132,385, sawa na asilimia 42 kati ya 50 iliyokusudiwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, halmashauri ya wilaya Pangani kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2024, ilikusanya chini ya malengo yake, kutokana na hali ya hewa ya baharini, ikiwemo upepo mkali ulioathiri uvuvi na ushuru unaotokana na mazao ya baharini.
Nayo halmashauri ya Jiji la Tanga iliyopangiwa Shilingi 21,060,272,000, ilifikia Shilingi 9,715,657,801 sawa na asilimia 46 kati ya 50 zilizotarajiwa.
Sababu ya kushindwa kufikia lengo ni kutolipwa ushuru wa madini yanayotokana na madini ya Iimestone na vifusi kutoka viwanda vya saruji.
Kwa hali hiyo, mapato ya mkoa wa Tanga kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 31, 2024, yalifikia Shilingi 23,053,472,275 sawa na asilimia 48 ya malengo ya Shilingi 47,554,027,000.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.