NA ESTHER MBUSI, OMT
Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima fomu ya mwongozo inayomtaka mwananchi yeyote ambaye hajaridhika na huduma za mahakama, ameona dosari yoyote au ana malalamiko kuyaorodhesha ili yafanyiwe kazi.
Akizungumza na RC Malima mkoani hapa Jumatatu Mei 16, Jaji Profesa Ibrahim amesema katika fomu hiyo mwananchi atatakiwa kuandika iwapo hajaridhika na huduma aliyokusudia kuipata, hakuridhika na lugha au hajatendewa haki katika maamuzi yaliyotolewa.
"Sisi huwa tuna kawaida ya kupokea mrejesho na bahati mbaya si wananchi wengi wanafahamu kwamba anapokuwa mahakamani kupata huduma lazima aridhike ambapo kama hajaridhika anaweza kujaza fomu iwapo hajaridhika na zile huduma aidha lugha au mwenendo anaweza kujaza fomu za malalamiko sisi tutaifanyia kazi.
"Kwa hiyo nikuombe Mkuu wa Mkoa, anaweza kuja mwananchi akalalamika kwako ukamjazia hii fomu ukaiwasilisha na sisi tutaifanyia kazi.
"Fomu hii pia inapatikana kwenye mtandao lakini sasa wananchi wengi wanalalamika kwenye mtandao hawawezi kufika kwa sababu ya bundle sasa wakija kwako au wakamkuta Katibu Tawala au maofisa wako wakajaza yale malalamiko kwa niaba yako zikatumwa kwa mtandao sisi tutaziona na kuzifanyia kazi.
"Kingine sisi huwa tunafanya shughuli zetu kimkakati kwa hiyo tuna mpango wetu mkakati ukiwa mdau wa mahakama utatuambia mkoa wangu kuna mkakati fulani sisi tunakusaidia..." amesema Jaji Profesa Juma.
Kwa upande wake RC Malima alisema Serikali ya Mkoa wa Tanga wana ushirikiano mzuri na mahakama isipokuwa changamoto kubwa ni suala la ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto.
Amesema ukatili wa kijinsia na unyanyasaji watoto unafanyika bila kificho lakini wanamalizana wenyewe ambapo hadi yeye akisikia jambo hilo anakuta wameshafanya michezo kwenye ushahidi ambapo kesi inakuwa ngumu kuisimamia.
"Lakini hilo ni jambo ambalo linatusumbua sana na nilichogundua linawasumbua wengi kwa sababu napata malalamiko mengi sana kutoka kwa wabunge wanawake na madiwani wa viti maalumu na wawakilishi wengine wa wanawake wanakuja kulalamika kuhusu vitendo hivyo, tunaiomba mahakama ikayasimamie haya," amesema RC Malima.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.