KIWANDA CHATOA ASILIMIA 90 YA AJIRA KWA WANAWAKE MUHEZA
Na Mashaka Mgeta, MUHEZA
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava, ameelezea kuvutiwa na takribani asilimia 90 ya ajira kwenye kiwanda kinachochakata mazao hai katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga, kuwa ni wanawake.
Mnzava ameyasema hayo leo, wakati Mwenge wa Uhuru 2024 ulipotembelea na kuzindua mradi wa mazao hai kwenye kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya GFP Organics Limited.
Amesema kuwepo kwa wawekezaji nchini, kunaashiria mazingira bora na salama yanayowekwa na Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ili kutoa fursa pana zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah, amesema kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda vikubwa vinne wilayani humo, vyenye fursa nyingi zikiwemo za kilimo cha matunda na viungo.
Mhe Zainab ametoa mfano kuwa, Muheza inazalisha takribani tano 300,000 za matunda kwa msimu mmoja, hivyo kuibua haja ya kuwekeza zaidi viwanda vya kuchakata matunda hayo.
Kwa upande wake, mmiliki wa kampuni ya GFP Organics Limited, Cleopa Ayo, amesema mradi huo uliogharimu Shilingi bilioni 2.7, ulianza kwa kuhamasisha wakulima kujiunga katika mfumo wa kilimo hai tangu mwaka 2004.
‘’Tunaelimisha na kujengea uwezo jamii jinsi ya kutekeleza kilimo hai na wanaofuzu, wanatengeneza kikundi ili kupata cheti cha kimataifa cha kilimo hai, na baadaye mazao yao kununuliwa na kuuzwa katika soko la kimataifa la bidhaa zinazotokana na kilimo hai,’’ amesema Ayo.
Ayo amesema miongoni mwa manufaa yaliyopo kupitia mradi huo ni kuwa na soko la uhakika la wakulima wa mazao ya viungo, machungwa na malimao wanaolima katika mfumo wa kilimo hai, ajira hasa kwa vijana na wanawake, ulipaji kodi ya mapato kwa Serikali Kuu, kodi ya huduma na ushuru wa mazao kwa halmashauri ya wilaya ya Muheza.
Mafanikio mengine ni uuzaji nje wa bidhaa za viungo kwa asilimia 100, hivyo kuingiza fedha za kigeni, kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuendeleza kilimo endelevu.
Ayo, ametoa mfano kuwa, mwaka 2020-2022 kupitia mradi wa New Origins Sustainable (NOSS) la Uholanzi, wakulima walipata elimu kuhusiana na kilimo endelevu, na kuanzishiwa vitalu vya miche ya viungo.
Amesema kwa sasa kuna mradi unaendelea kwa ubia kati ya GFP na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) wa uanzishwaji wa vitalu vya miche ya mazao viungo na miti maji, mafunzo katika nyanja za kilimo endelevu, hifadhi ya maji na udongo na uanzishwaji wa vikundi vya kifedha vya kijamii.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.