Watu 148,157 katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Afisa Uchaguzi wa Halmashauri hiyo, Mwanaamina Mruma, amesema hayo wakati Mwenge wa Uhuru 2024 wenye ujumbe unaosema, ‘Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu’ ulipotembelea na kukagua kituo cha kupigia kura cha kata ya Kagunda, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi huo.
Mruma amesema hadi kufikia jana Jumatatu, halmashauri hiyo imefanya kazi kadhaa zikiwemo uhakiki wa maeneo ya utawala yatakayohusika kwenye uchaguzi huo, yatakayotangazwa rasmi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwenye Gazeti la Serikali.
Pia amesema halmashauri imehakiki vituo 610 vya kuandikishia orodha ya wapiga kura na baadaye kuwa vituo vya kupigia kura katika kata 29, vijiji 118 na vitongoji 610.
Mruma amesema hadi kufikia sasa, halmashauri hiyo ina masanduku ya kupigia kura 1,199 kati ya 2,380 na mihuri ni 118 kati ya 610 inayohitajika.
Kwa mujibu wa Mruma, halmashauri hiyo imetenga Shilingi milioni 30 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya uchaguzi huo, wakati Shilingi 1,077,640,296 zinatarajiwa kutoka Serikali Kuu.
Ili uchaguzi huo kuwa na ufanisi zaidi, Mruma anasema halmashauri ya wilaya ya Korogwe inatekeleza mikakati kadhaa ya kutoa elimu kwa umma kugombea na kushiriki uchaguzi huo.
Mikakati hiyo ni pamoja na kutumia mikutano wa hadhara kwenye ngazi za wilaya, tarafa nne, kata 29, vijiji 118 na vitongoji 610 vilivyopo wilayani Korogwe, kuandaa na kusambaza vipeperushi, mabango na stika za hamasa, kutumia vikundi vya nyimbo, ngoma, maigizo, mashairi, magari ya matangazo na redio.
Habari hii imeandikwa na Mashaka Mgeta wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.