LISHE YAZIDI KUIMARIKA TANGA, UDUMAVU WAPUNGUA KWA KASI
HALI ya lishe katika mkoa wa Tanga imeendelea kuimarika, ambapo takwimu zinaonyesha kupungua kwa kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 34 mwaka 2018 hadi 24 mwaka 2024.
Aidha, kiwango cha uzito pungufu kimepungua kutoka asilimia 15.6 hadi 11.2 katika kipindi hicho, ikiwa ni ishara kwamba juhudi za kuboresha lishe zimezaa matunda.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, ameeleza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kuweka msukumo mkubwa kuhakikisha lishe bora inazingatiwa katika jamii, ili kupambana na utapiamlo.
Hata hivyo, Mhe Balozi Dk Batilda, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa jamii, ili kukabiliana na ongezeko la ukondefu kwa watoto, ambalo limepanda kutoka asilimia 2.7 hadi 5.6.
Amesema, tatizo hilo linachangiwa na watoto kusumbuliwa na maradhi yanayopunguza hamu ya kula na baadhi ya wanawake kushindwa kunyonyesha watoto wao kwa usahihi.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa Tanga, Pili Mnyema, amesema Serikali imewekeza katika kuimarisha nyanja ya lishe kwa kuajiri maafisa lishe katika halmashauri zote za mkoa huo.
Amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kushindwa kutekeleza kikamilifu afua za lishe, kwani mkoa huo una wataalamu wa kutosha kuhakikisha wananchi wanapata elimu na huduma sahihi za lishe.
Amesema, juhudi hizo zinaendelea kuboresha afya na ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla, huku serikali ikihamasisha ushirikiano kati ya wadau mbalimbali ili kuhakikisha mafanikio zaidi katika sekta ya lishe.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.