Serikali Mkoani Tanga imesema itaendelea kuwaunganisha watumishi wa umma pamoja na taaasisi zilizopo mkoani humo kupitia michezo ili kujenga mahusiano na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Pili Mnyema katika bonanza la michezo Kwa watumishi wa idara na taasisi za umma mkoani Tanga.
Akizungumza Mnyema amesema michezo ni sehemu ya kuwakutanisha pamoja watumishi ambao muda mwingi wanautumia ofisini kuwatumikia wananchi.
“Undugu, ujamaa unatengenezwa baina yetu kupitia michezo kwa hiyo majumuiko kama haya ni sehemu ya kuendelea kutusogeza pamoja kama familia” alisema Mnyema.
Pia Mnyema amesema michezo ni uchumi hivyo vijana watumie fursa hiyo kujiunga na michezo mbalimbali itayowafanya wajulikane katika maeneo mbalimbali.
“Vijana wetu ambao bado mpo mashuleni tumieni fursa hii tunaona katika miaka ya hivi karibuni hatuwezi kutaja watu waliofanikiwa bila kutaja wanamichezo” aliongeza Mnyema.
Sambamba na hilo katibu tawala Mkoa wa Tanga amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka nguvu nyingi kuhakikisha michezo ndani ya taifa letu inakua na kuimarika zaidi.
Kwa upande wake afisa michezo mkoa wa Tanga Digna Tesha amesema mkoa umejipanga kuhakikisha michezo kama hiyo inafanyika kila robo ya mwaka ili kuendeleza desturi nzuri iliyoanzishwa katika kujenga uhusiano baina ya watumishi wa umma na taasisi kupitia michezo.
Kwa upande wa washiriki waliohudhuria bonanza hilo wameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa kuandaa bonanza hilo ambalo limeleta matokeo mazuri.
Taasisi zilizoshiriki bonanza hilo la michezo ni TRA, TANESCO, GIPSA, Bodi ya Mkonge, SISALANA, Magereza,Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa, Jeshi la zimamoto, NMB,Bonde la maji Pangani, TAKUKURU, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo,TANGAUWASA, Uhamiaji,TPA,Vilabu vya michezo pamoja na shule mbalimbali za mkoa wa Tanga.
Imeandaliwa na Emma Kigombe, Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.