Na Mashaka Mgeta, PANGANI
MRADI wa maji unaogharimu Shilingi milioni 500, wenye kuwahudumia watu zaidi ya 2,500 kwenye kaya 600 katika kijiji cha Tuangamaa, umeiwezesha wilaya ya Pangani mkoani Tanga kufikisha asilimia 86.5 ya upatikanaji maji kutoka asilimia 83.5 iliyokuwepo awali.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga, Mhandisi Upendo Lugongo, amesema hayo jana Aprili 15, 2025 wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mhe Gift Msuya.
Mhandisi Lugongo amesema mradi huo ulioanza mwaka 2024, ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika sekta ya maji inayoelekeza upatikanaji maji maeneo ya vijiji kuwa asilimia 85 na mijini kwa asilimia 95.
Amesema mradi huo unahusisha miundombinu bora ya usambazaji maji inayowawezesha wakazi wa Tungamaa wanaofikia 2,047 kupata huduma hiyo katika vituo vya jamii 13 ama kuingiza kwenye makazi yao.
Naye Meneja wa RUWASA wilaya ya Pangani, Mhandisi Rajab Yahaya amesema kabla ya mradi huo, wakazi wa Tungamaa walikabiliwa na changamoto ya upungufu wa maji safi na salama kutokana na uliokuwepo awali, kukidhi asilimia 20 ikilinganishwa na sasa wenye kufikisha zaidi ya asilimia 100.
Mhandisi Yahaya amesema awali, mahitaji ya maji kijijini humo yalikuwa lita 60,000 lakini kupitia mradi wa awali, kiasi cha lita 20,000 pekee kilizalishwa, lakini sasa kiwango hicho kimeongezeka kupitia mradi mpya, kufikia lita 120,000 kwa siku, wakati mahitaji ni lita 61,000 kwa siku.
Akizungumza kwa niaba ya Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mhe Msuya amesema, kasi ya upatikanaji maji wilayani humo inatoa mwelekeo wa ifikapo Disemba 2025, maeneo ya mijini na vijijini yatakuwa na zaidi asilimia 100.
Mhe Msuya amesema, hatua hiyo inatokana na uwepo wa miradi mikubwa saba inayotekelezwa kwenye maeneo ya vijijini na sehemu ya mradi wa miji 28 unaozinufaisha pia wilaya za Korogwe, Handeni na Muheza.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.