Na Mashaka Mgeta, ZANZIBAR
WAPO wanaomtambua kwa ufasaha wa lugha hasa Kiswahili, wengine wanamjua zaidi kwa umahiri wa imani na mapokeo ya dini, sasa amedhihirisha sehemu ndogo ya namna anavyoielewa Zanzibar.
Huyo si mwingine, bali ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Profesa Paramagamba Kabudi, aliyefika Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka 1978, akiwa Mwandishi wa Habari. Imefika takribani miaka 47.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe Hemed Suleiman Abdulla, kufungua Kikao Kazi cha 20 cha Maafisa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na Itifaki Aprili 3, 2025 mjini Unguja, Mhe Profesa Kabudi, akaeleza anavyoifahamu historia ya Zanzibar iliyo sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe Abdulla alifungua Kikao Kazi hicho kwa niaba ya Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Mhe Profesa Kabudi akasema, kwa kipindi chote hicho, hakujawahi kuwepo kasi kubwa ya maendeleo, ikiwemo miundombinu na ustawi wa watu wa Zanzibar kama sasa, chini ya uongozi wa Mhe Dkt Mwinyi.
Akatoa mfano kuwa, miongoni mwa viashiria vya ukuaji maendeleo ya Zanzibar ni miundombinu inayofungamana na kuchochea shughuli na ukuaji wa uchumi.
Hapo, akaibua historia ya reli iliyokuwepo awali, ikitoa huduma za usafiri na usafirishaji kutoka maeneo ya katikati ya Unguja kwenda Bububu, jina lenye asili inayotokana na kelele za ‘bu-bu-bu…’ zilizotoka kwenye treni iliyotumia reli hiyo.
Historia hiyo ikamvutia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulidi Mwita ambaye - kwa mujibu wa Mhe Abdulla, alionesha kushangazwa na ufahamu wa Mhe Profesa Kabudi kuhusu historia ya Zanzibar.
Akifungua Kikao Kazi hicho, Mhe Abdulla, pamoja na mambo mengine, akagusia hoja ya Mhe Profesa Kabudi kuhusu Bububu, akasema hivi sasa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ipo kwenye mchakato wa kujenga reli hiyo, itoe huduma bora na za kisasa.
Mhe Abdulla akasema, utaratibu wa mchakato huo umeshaanza, kisha akathibitisha kwa Mhe Profesa Kabudi kuwa ‘ndoto yake’ kuhusu kurejea kwa reli hiyo itatimia inshallah.
Naye Mhe Mwita akamtaja Mhe Profesa Kabudi kama ‘maktaba inayotembea’, na kwamba ushirikiano wa wizara wanazoziongoza, uliowezesha kufanyika kwa Kikao Kazi cha 20 huko Unguja ni ishara ya kuzidi kuimarika kwa Muungano.
Mhe Mwita akasema Kikao Kazi hicho kimewaweza washiriki kuyaona maendeleo yalifikiwa Zanzibar, kushiriki utalii wa ndani, kuendeleza na kudumisha ushirikiano wa kabla na baada ya Muungano wa Aprili 26, 1964.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.