Na Mashaka Mgeta, MOROGORO
MUASISI wa jukwaa la Jamii Forum ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi wa Jamii Afrika, Maxence Melo, ametoa rai kwa waandishi wa habari kuandika na kuzitangaza hatua za maendeleo yaliyofikiwa na yanayotokea nchini, kupitia vyombo vya habari vya kikikanda na kimataifa.
Melo, amesema wajibu huo unapaswa pia kutekelezwa na Maafisa Mawasiliano, Habari na Uhusiano wa Serikali kutokea kwenye taasisi zao.
Melo ametoa rai hiyo Aprili 11, 2025, alipokuwa akizungumza kwenye mjadala wenye mada iliyosema. “Mustakabali wa mawasiliano ya Serikali, Mwelekeo, Changamoto na Fursa.”
Mjadala huo na mingine kadhaa, ilikuwa sehemu ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) ulifanyika mjini Morogoro kuanzia Aprili 8 hadi 12, 2025.
Melo amesema. yapo mafanikio na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na yanayoendelea kufanyika kwenye sekta tofauti, ikiwemo miundombinu na kasi kubwa ya ukuaji wa miji na majiji.
Ametoa mfano wa miradi husika kuwa ni reli ya kisasa (SGR) yenye mtandao usiopungua Kilomita 2,561, ikiunganisha mikoa kama vile Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Tanga, Mara, Katavi na nchi zisizokuwa na bandari zikiwemo Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mwingine ni Mradi Kufufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, miundombinu ya mawasiliano kama barabara kwenye miji ikiwemo Dar es Salaam, miongoni mwa mengine mengi.
Amesema, habari zinazohusu maendeleo hayo na ustawi wa maisha ya Watanzania, zinapaswa kuchapishwa na kutangazwa kwa kasi kubwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kikanda na kimataifa.
Melo amesema kama maafisa hao watashindwa kuzitumia taarifa nyingi na nzuri zilizopo kwenye taasisi zao, wapotoshaji watatumia mwanya huo kutimiza malengo ama nia ovu kwa kuchapisha taarifa zisizo sahihi.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen, aliyechangia mada hiyo.
Dausen akasema, tofauti za mitazamo na fikra kuhusu maendeleo na ustawi wa watu, haviwezi kukosekana ndani ya nchi, lakini kwa mukhtadha wa kikanda na kimataifa, raia wote hasa wana habari wana wajibu wa kuyatangaza mambo mema ya nchi.
Amesema, kuandika na kutangaza mambo mazuri ya Tanzania kunapaswa kufanyika kupitia matumizi ya takwimu sahihi zinazothibitisha viwango vya maendeleo na ustawi wa watu, ili kukabiliana na upotoshaji dhidi ya ukweli uliopo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Nteghenjwa Hosseah, amewahimiza Maafisa Mawasiliano, Habari na Uhusiano wa Serikali, kuitumia mitandao yenye kuifikia sehemu kubwa ya watu ulimwenguni, ikiwemo Jamii Afrika, ili kujua, kujadili, kujibu hoja na kutangaza maendeleo na mambo mema yaliyopo nchini.
Pia Nteghenjwa amesema ipo haja ya kuendelea kuwajengea uwezo na kuwapa motisha Maafisa hao, ili watimize wajibu huo muhimu kwa maslahi ya nchi na watu wake.
Nteghenjwa ametoa rai kwa Maafisa Mawasiliano, Habari na Uhusiano wa Serikali, kujenga utamaduni wa kusoma, kuandika, kuchakata na kuzitafsiri taarifa mbalimbali kwa mujibu wa nyaraka zinatoa mwelekeo wa maendeleo nchini.
Ametoa mfano wa nyaraka hizo kuwa Mpango nyaraka hizo kuwa ni Mpango wa Maendeleo wa Taifa, sera mbalimbali, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dira ya Taifa na Miongozo mbalimbali ya Serikali.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.