Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewaita Maafisa Habari, Mawasiliano, Uhusiano na Itifaki Serikalini, kushiriki Kikao Kazi cha 20 kitakachofanyika Unguja, Zanzibar kuanzia Aprili 3 hadi 6, 2025.
Wito wa Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, umetolewa leo Machi 18, 2025 na kusambazwa na Idara ya Habari (MAELEZO), ukieleza kuwa washiriki wa Kikao Kazi wanatoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Kwa mujibu wa Msigwa, Kikao kazi hicho kinaratibiwa na MAELEZO, Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali (SMT) kwa kushirikiana na Idara ya Habari-MAELEZO (SMZ).
Msigwa amesema wakati wa Kikao kazi hicho, kutatolewa huduma za upimaji afya na matibabu kwa washiriki, waandishi wa habari, watoto na watu wazima bila malipo.
Huduma na matibabu hayo vitatolewa na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Taarifa hiyo ya MAELEZO imeleeza, huduma za afya zitatolewa wakati wote wa kikao kazi hicho kuanzia saa 3:00 hadi 11:00 jioni kwenye uwanja wa New Amani Complex.
MAELEZO kupitia taarifa hiyo imeainisha huduma zitakazotolewa na MNH ni upimaji na uchunguzi wa figo, kisukari, macho na afya ya akili na kutoa elimu kuhusu magonjwa hayo na saratani, lishe bora na upimaji wa afya ya lishe.
Kwa upande wa JKCI itatoa huduma za uchunguzi wa kuangalia mfumo wa umeme wa moyo, shinikizo la damu, wingi wa sukari kwenye damu, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na uwiano baina na urefu na uzito.
Pia JKCI itatoa elimu kuhusu magonjwa ya moyo, lishe bora na matumizi sahihi ya dawa za moyo.
Nayo MOI itafanya uchunguzi wa magonjwa ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, na kuelimisha kuhusu magonjwa ya mifupa, ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu, mazoezi tiba, ukaaji na ulalaji sahihi ili kujiepusha na maumivu ya mgongo.
“Huduma hizi ni sehemu ya huduma kwa jamii zinazotolewa kwa ushirikiano wa hospitali hizi za kitaifa na Waratibu wa Kikao Kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Uhusiano na Itifaki wa Serikali,’ imehitimisha taarifa hiyo.
Mwisho.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.