MWANAMKE ATOA ENEO LAKE KWA UJENZI WA MRADI WA MAJI BUMBULI
MKAZI wa kijiji cha Funta katika halmashauri ya Bumbuli wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Amina Idd, ametoa mita za mraba 17 kutoka eneo la makazi yake kwa ajili ya mradi wa maji kwa wakazi wa eneo hilo uliowekewa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru 2024 jana.
Hatua hiyo imefikiwa na mkazi huyo ili kukabiliana na ukosefu wa eneo uliosababisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilaya ya Lushoto, kupata changamoto ya kupata mahali panapofaa kwa ajili ya ujenzi wa tenki lenye ukubwa wa lita za ujazo 120,000, ili litumike kutoa huduma ya maji kwa wakazi zaidi ya 4,000 wa kijiji hicho na maeneo ya jirani.
Mradi huo ulifunguliwa jana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 wenye ujumbe unaosema, ‘’Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu,’’ Ndugu Godfrey Mnzava.
‘’Niliwaona RUWASA wakihangaika kutafuta eneo la kujenga mradi wao huu, waliponifuata na kutokana na kero ya maji iliyokuwepo awali, nikaona hakuna sababu ya kushindwa kutoa sehemu ya kiwanja change hiki kidogo, itume kwa mradi wa maji wenye maslahi kwa watu wengi zaidi,’’ anasema Amina.
Kwa mujibu wa Amina na uthibitisho wa uongozi wa RUWASA wilayani Lushoto, eneo hilo limetolewa bure, na kwa kutambua utayari wake huo, (Amina) aliunganishiwa huduma ya maji bure.
Faidha Adam ni mkazi wa kijiji hicho, anasema ukosefu wa maji uliwasababishia kadhia nyingi ikiwemo kuharibika kwa mahusiano kwenye ndoa, ikiwemo baadhi ya wanaume kutowaamini wake zao waliotumia muda mrefu kwenda maeneo ya mbali kutafuta maji.
Naye Angela Yusuph wa kijiji hicho anasema, ukosefu wa maji uliwasababishia kero ya kupanda milima ili kuyafikia maeneo yenye vyanzo vya maji, hukuwa wakishindwa kumudu mahitaji ya usafi wa mwili na mazingira.
Meneja wa RUWASA mkoa wa Tanga, Mhandisi Upendo Lugongo, anasema mradi huo ulioanza kujengwa Agosti 18, 2022 na kutarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 Aprili 30 2024, umegharimu takribani Shilingi milioni 833.
Habari hii imeandikwa na Mashaka Mgeta wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.