MWENGE WAWAAGIZA WAKUU WA WILAYA KUHUSU HIFADHI YA MAZINGIRA
Na Mashaka Mgeta, Tanga
KIONGOZI wa Mbio wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Godfrey Mnzava, amewaelekeza Wakuu wa Wilaya ambazo Mwenge huo utapita kwenye halmashauri zao, kuhakikisha ajenda ya hifadhi wa mazingira inasimamiwa kwa vitendo na uendelevu.
Pia amesema viongozi hao wanapaswa kuandaa na kuwasilisha mipango madhubuti waliyoiweka kuhakikisha kwamba wananchi wanashiriki na kutumia haki zao kikatiba kushiriki, kugombea na kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Mnzava amesema, suala la upandaji miti unaofanywa na Mwenge wa Uhuru ikiwa ni ishara ya hifadhi ya mazingira nchini, halifanyiki kwa mazoea, bali kujali uhalisia na maana ya upandaji miti inayopaswa kutunzwa ili ikue na kudumu.
‘’Ninaagiza huko tunapokuja, hakikisheni miti inayopandwa siyo kwa ajili ya wakimbiza Mwenge tu…tunataka watu washiriki kupanda miti kwa wingi wao na kabla ya hapo, tuione miti iliyopandwa ili pamoja na hii tunayoipanda ikue na kudumu,’’ amesema.
Mnzava ameyasema hayo baada ya kutembelea, kukagua na kuridhika na mradi wa dampo la kisasa lililopo eneo la Mpira, kata ya Chongoleani mkoani Tanga, na kutoa wito kwa mamlaka za mikoa na serikali za mitaa zinazotaka kujifunza kuhusu hifadhi ya mazingira, kuja mkoani humo.
Taarifa ya halmashauri ya jiji la Tanga kwenye mradi huo, imeeleza kuwa kushirikiana na wadau wake, hadi kufikia Aprili mwaka huu, wamepanda miche 240,365 ya vivuli, mbao, matunda na miti 80,543 ikiwemo mikoko, mbao, matunda na kivuli.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF), wananchi wameweza kuibua miradi ya upandaji miti ambapo iliyopangwa ni 10,000.
‘’Zoezi la upandaji miti ni endelevu ambapo wananchi wamepewa maarifa ya kupanda miti mbalimbli na pia wameendelea kuelimishwa mbinu za kuitunza kupitia kamati za mazingira za Mitaa na pia kupitia kampeni ya soma na mti kwa upande wa taasisi za elimu,’’ imeeleza taarifa hiyo.
Kwa upande mwingine, taarifa hiyo imeeleza kuwa kupitia mpango wa kufanya usafi wa mazingira na kuondosha taka, jiji la Tanga limetengeneza ajira za muda 152 na sehemu kubwa ikiwahusu vijana.
Taarifa hiyo imeeleza,’’wananchi huhamasishwa kuishi katika mazingira yaliyo safi wakati wote, na pia kushiriki kwa pamoja kufanya usafi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi maarufu kama msaragambo.’’
Dampo lililokaguliwa na Mwenge wa Uhuru kuridhika katika nyanja ya hifadhi ya mazingira, ndipo zinapowekwa taka kutoka kwenye maeneo tofauti yakiwemo makazi na viwandani jijini Tanga.
Aidha, katika udhibiti wa taka ngumu, wadau mbalimbali wanaofanya shughuli za urejerezaji, watambuliwa na kupewa ushirikiano unaowawezesha kuwa na mchango mkubwa kwenye udhibiti taka na usafi wa Jiji ambapo wastani wa tani 176 za taka hudhibitiwa kwa siku.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kushirikiana na Bonde la mto Pangani, Marine park na wadau wengine, Tanga inatekeleza programu mbalimbali za uhifadhi wa vyanzo vya maji ambapo mikoko 12,700 na miti 1,750 imependwa kwenye vyanzo viwili vya maji vilivyopo ndani ya jiji hilo.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.