MWENGE WAWEKE HISTORIA, WAFUNGUA MADARASA YA KIDATO CHA TANO NA SITA PANGANI
Na Mashaka Mgeta, PANGANI
KASI ya kutanua wigo wa huduma za jamii ikiwemo elimu nchini, inazidi kuongezeka, huku Shule ya Sekondari ya Funguni katika wilaya ya Pangani mkoani Tanga, imeingia kwenye historia ya kuwa na madarasa ya kidato cha tano na sita ambayo tangu kuanzishwa kwake, hayakuwepo.
Mwenge wa Uhuru 2024 wenye ujumbe unaosema ‘’Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu’’, umeingia wilayani Pangani leo na miongoni mwa miradi inayoutembelea ni ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu saba ya vyoo kwenye shule hiyo.
Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Nassoro Gamba anasema, kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kwa mara ya kwanza kwenye historia ya shule hiyo, kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita kwa michepuo ya HGL na HGE.
Amesema, ujenzi huo ulianza Januari 29, 2024 na kukamilika Machi 28, 2024, ukiwa na thamani ya Shilingi 117,645,525.00 ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi 100,000,000 ni gharama za ujenzi wa madarasa manne, Shilingi 16,000,000 za ujenzi wa matundu saba ya vyoo na Shilingi 1,645,525 ni thamani ya nguvu za wananchi.
Gamba amesema, hadi sasa, Shilingi 117,645,525 zimetumika kwa ujenzi zikihusisha usafishaji wa eneo, kuchimba msingi, kuingiza mawe, kumwaga jamvi la zege, kuchimba mashimo ya choo na nguvu za wananchi zilizothamanishwa kwa Shilingi 1,645,525.00.
Pia Shilingi 100,600,000 za gharama za ujenzi, Shilingi 12,400,000 zikiwa ni gharama za ufundi kwa vyumba vinne vya madarasa na Shilingi 3,000,000 za ufundi wa ujenzi wa matundu saba ya vyoo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Mnzava, ameridhishwa na mradi huo, kwamba umetekelezwa na kufikia malengo yake na hivyo akauzindua.
Akizungumzia umuhimu wa elimu ya vita dhidi ya rushwa, Mnzava amesema taifa linaendelea kukabiliwa na watu wasiokuwa na nia njema, wanaojihusisha na vitendo hivyo, hali inayochangia kupotea kwa haki na upotevu wa maadili.
Mnzava amesema wapo watumishi na viongozi katika sekta za umma na binafsi wanaoweka vikwazo katika utoaji huduma kama kishawishi cha kupewa rushwa na wahitaji.
‘’Ninatoa wito kwa wananchi wote tushiriki kikamilifu kupiga vita rushwa,’’ amesema na kuongeza kuwa suala la kujielimisha kuhusu mbinu za kuzuia na kupambana na rushwa linapaswa kuwa endelevu.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.