Na Mashaka Mgeta, ZANZIBAR
NI hotuba iliyoandikwa kwa weledi, ikasomwa kwa utulivu, ukumbi wa hoteli ya New Amaan mjini Unguja ukitumika kwa mara ya kwanza tangu uzinduzi wa mara ya pili ya miundombinu ya huduma na michezo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex ulipofanyika Disemba 26, 2024.
Maafisa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, walikusanyika kwenye ukumbi wa hoteli hiyo kushiriki Kikao Kazi cha 20 kilichofanyika mjini humo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe Hemed Suleiman Abdulla, akapewa jukumu la kumwakilisha Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kufungua kikao hicho kilichoanza Aprili 3 hadi 6, 2025.
Ubora wa hotuba na uwasilishaji wake, vikaongeza chachu ya usikivu ukumbini, na hivyo kuyabaini kwa ufasaha maeneo yote ikiwemo nasaha za kuzitaka taasisi za umma, kuendelea kuyaboresha mazingira ya utendaji kazi wa Maafisa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali, ili watimize majukumu yao ipasavyo.
UBORA WA MAUDHUI
Kupitia hotuba, Mhe Rais Dkt Mwinyi akatoa mfano kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, Maafisa hao wana wajibu wa kuhakikisha ubora wa maudhui ya habari zinazowafikia wananchi, ili wafanye uamuzi sahihi katika kuwachagua viongozi wanaofaa.
Akasema, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinatambua kuwa maafisa hao wana dhima ya ushauri kwa viongozi wa taasisi za umma, hususani kwa masuala yanayohusu hoja zinazoibuka kwenye jamii na kuhitaji mrejesho kutoka serikalini.
Amewataka Maafisa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kuhakikisha kuwa taarifa wanazozikusanya, kuzichakata, kuzichapisha na kuzitangaza zinaufikia umma kwa wakati na usahihi.
Amesema hatua hiyo inatoa mwanya kwa wananchi ambao walio wengi wanatambua utekelezaji wa miradi ya maendeleo unavyogusa mahitaji yao, kufanya tathmini na kufikia uamuzi sahihi Uchaguzi Mkuu utakapofanyika.
UBUNIFU NA USHIRIKIANO
Pia, amewaasa Maafisa hao kuwa wabunifu na wenye kutanua zaidi wigo wa njia za upashaji habari kwa umma, ili kuwawezesha wananchi kutambua hatua kubwa ‘zilizopigwa’ kupitia miradi ya maendeleo inayostawisha maisha yao, kuchochea haki, usawa na misingi ya demokrasia na utawala bora nchini.
Kwa upande mwingine, Mhe Rais Dkt Mwinyi, amesema Maafisa hao wanapaswa kushirikiana kwa karibu na Waandishi wa Habari wa vyombo vya Serikali na binafsi, ili kuwezesha utoaji taarifa zilizo sahihi, kwa wakati na hivyo kuepusha migogoro inayoweza kusababishwa na ukosefu wa taarifa husika ama upotoshaji.
Amesema, Sserikali mbili hizo zimetekeleza kwa vitendo ahadi zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025 kwa kuanzisha na kuendeleza miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi wote.
AVIPONGEZA VYOMBO VYA HABARI
Mhe Rais Dkt Mwinyi, amevipongeza vyombo vya habari vya Serikali na binafsi kwa kutimiza wajibu wa kutoa taarifa sahihi kwa umma hasa kuhusu hatua za maendeleo zilizofikiwa na zinazoendelea kufikiwa nchini.
Amewaasa Maafisa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na Itifaki kutumia mijumuiko na mahali pa kazi ujadiliana na kujifunza ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
TAARIFA ZIWAFIKIE WANANCHI KWA WAKATI
Mhe Rais Dkt Mwinyi amesema kuwepo kwa miradi mikubwa ya ki-mkakati kama ujenzi wa mitambo ya umeme wa megawati 2115 utakaounganishwa kwenye gridi ya Taifa na kuongeza viwango vya matumizi ya nishati hiyo viwandani na majumbani kunastahili kujulikana vema kwa wananchi.
Ametaja miradi mingine kuwa ni SGR, wakati visiwani Zanzibar kuna Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amaan Abeid Karume na uboreshaji bandari zikiwemo za Malindi, Mkoani, Wete, Mangapwani na Shumba Mjini.
MAAGIZO
Kupitia kikao hicho, ameagiza taasisi zote za Serikali ziandae mikakati ya mawasiliano, kuwajengea uwezo maafisa hao kutumia teknolojia za kisasa za habari na mawasiliano, kuwawezesha kwa vitendea kazi bora, kuwashirikisha kwenye masuala yote yanayohusiana na miradi ya maendeleo.
Maagizo mengine ni kujenga mahusiano mazuri na vyombo vya habari vya sekta binafsi na kufanya kazi kwa misingi, kanuni na taratibu zinazoongoza tasnia hizo pasipo ‘kufanya kazi kwa mazoea’.
MSIGWA: TUSIWE KIKWAZO KWA WAANDISHI
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewataka Maafisa hao wasiwe kikwazo kwa Waandishi wa Habari kupata taarifa zinazohusiana na taasisi za umma hususani katika maeneo ya miradi ya maendeleo.
Amesema miongoni mwa majukumu msingi ya Maafisa hao ni kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka kwenye taasisi za umma kwenda kwa wananchi, kupitia vyombo vya Habari.
Msigwa amesema, utekelezaji wa jukumu hilo inaweza kurahisishwa zaidi na uwepo wao (Maafisa) kwenye klabu za Waandishi wa Habari ngazi ya mikoa.
Amesema kuwepo kwa maafisa hao kwenye vilabu hivyo kutawarahisishia na kuwawezesha kujua mahitaji halisi, na changamoto zinazowakabili Waandishi wa Habari na namna ya kukabiliana nazo, ikibidi kwa kuwahusisha wakuu wa taasisi husika.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.