Na Mashaka Mgeta, Kilindi
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Waziri Kindamba ametumia dakika 17 kumaliza mgogoro uliodumu kwa miaka 17 ukihusisha mpaka kati ya vijiji vya Gitu na Ngobole Wilayani Kilindi.
Hatua hiyo imefikiwa na Mhe. Kindamba aliyefuatana na Kamati ya Usalama (KU) ya Mkoa wa Tanga na Katibu Tawala Mkoa, Pili Mnyema.
Mgogoro huo ulihusu mpaka wa kijiji cha Gitu na Ngobole ambapo vitongoji vilivyokuwa na mgogoro ni Komtindi na Ng'aloji ambavyo vimesajiliwa kijiji cha Gitu, ila mpaka wa ramani ya upimaji wa vijiji hivyo ulipoainishwa ardhini ilibainika vitongoji hivyo kuwa katika Kijiji cha Ngobole.
Akionekana kukerwa na mgogoro huo uliotajwa pia na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokutana hivi karibuni na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mkoa, Mhe. Kindamba akasema, kwa mujibu wa tamko rasmi la Serikali (GN), vitongoji hivyo vipo katika kijiji cha Gitu.
Ameuagiza uongozi wa Gitu na Ngobole kuandaa muhtasari wa mkutano aliotoa agizo hili ili kuweka kumbukumbu kwenye mamlaka husika.
Mhe. Kindamba amesema haiwezekani kwa mkoa wa Tanga unaopokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo kutoka kwa Mhe. Dk Samia, ushindwe kujikita kwenye maendeleo ya ustawi wa wananchi, badala yake ubaki kushughulikia migogoro isiyokuwa na tija kama wa mpaka unaotambuliwa na GN.
Mhe. Kindamba ameiagiza halmashauri ya Wlĺ4ilaya ya Kilindi, kwa usimamizi wa Mkuu wa Wilaya hiyo, kuweka alama za kudumu za kutenganisha maeneo ya vijiji hivyo.
Pia, Mhe. Kindamba amesema eneo la takribani hekta 2000 lililopo kwenye eneo hilo limekabidhiwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili walitumie kwa mazoezi ya ulinzi na usalama.
Amesema JWTZ iliwahi kuliomba eneo hilo muda mrefu, lakini ombi lao bado halijashughulikiwa.
Mhe. Kindamba akatumia fursa hiyo kuwaonya viongozi wa vijiji hususani wenyeviti wilayani Kilindi na kwingineko mkoani Tanga, kuacha kujihusisha na uuzaji holela ya maeneo ya vijiji vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
"Viongozi tunapaswa kuwatumikia wananchi badala ya kujinufaisha binafsi, tufuate Sheria, Kanuni na Taratibu...hali ya Kilindi katika maeneo hayo haipo vizuri," ameonya.
Mhe. Kindamba akawataka wananchi wa Kilindi kuepuka migogoro ya ardhi inayowafikisha kupigana na kupeana majeraha.
MWISHO.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.