Na Emma Kigombe, OMM TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, leo Julai 12, 2025, amemkabidhi gari Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe Salum Nyamwese, ikiwa ni gari la saba kati ya manane yanayokabidhiwa kwa wakuu wa wilaya zote za mkoa huo.
Mhe Balozi Dkt Batilda ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa viongozi wa mkoa huo, hatua ambayo itawawezesha kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Amesema magari hayo yatasaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya viongozi hao, hususan katika kufuatilia miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati, na kuongeza uwajibikaji katika maeneo yao ya kiutawala.
“Gari hili litakuwa msaada mkubwa tukizingatia kuwa Wilaya ya Handeni ni kubwa na baadhi ya maeneo yake ni vigumu kufikika. Tunaamini litamuwezesha Mkuu wa Wilaya kuwafikia wananchi wake kwa urahisi zaidi,” amesema Mhe Balozi Dkt Batilda.
Kwa upande wake, Mhe Nyamwese, ameishukuru Serikali kwa kumpatia gari hilo, akibainisha kuwa litakuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi wa Handeni.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.