RC TANGA ATAKA MAENEO YENYE MIGOGORO YASIUZWE
Na Emma Kigombe
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba amepiga marufuku uuzwaji wa ardhi kiholela na usio rasmi katika maeneo yenye migogoro.
Mhe Kindamba amepiga marufuku hiyo wilayani Kilindi wakati akikagua eneo la mpaka wa kijiji cha Gitu na kijiji cha Ngobole kilichopo wilayani Simanjiro ambalo limekuwa na changamoto ya mgogoro wa ardhi kwa takribani miaka 17 ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea wilaya zote za mkoa huo na kuzungumza na watumishi pamoja na kamati ya fedha na uongozi.
“Haya maeneo yenye mgogoro yasiuzwe, lakini zipo taarifa zinazoonesha haya maeneo yenye mgogoro yanauzwa peleka ujumbe huu kwa wote wanaohusika yeyote atakaye uza na tukathibitisha tutamchukulia hatua kwa mujibu wa sheria taratibu na kanuni hatutaangalia ukubwa wake wala cheo chake” alisema RC Kindamba
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba akatumia nafasi hiyo kuwataka wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wa Kijiji na kata ambao wanahusika kuuza ardhi bila ya kufuata utaratibu uliowekwa kisheria.
“kiongozi yoyote ambae atathibitika kwa makusudi kuuza kwa mara ya pili maeneo ambayo yanamigogoro ya ardhi hatutamuonea haya tutamchukulia hatua” aliongeza Rc Kindamba.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa wa Tanga mhe. Waziri Kindamba amewataka viongozi wilayani Kilindi kukaa na kumaliza migogoro ndani ya wilaya yao ikiwemo migogoro ya Kijiji na Kijiji na wilaya kwa wilaya ili kuepuka kupoteza muda mwingi kufanya suluhu na badala yake kujikita katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
“mpaka kufikia Julai mosi mwaka huu 2023 nataka kusikia migogoro yote iliyopo baina ya kijiji na kijiji, wilaya kwa wilaya inamalizika ili mwaka mpya wa fedha unapoanza tujikite katika masuala ya maendeleo” alisema Rc Kindamba
Wilaya ya kilindi ni ya Saba kutembelewa na mkuu wa mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba tangu alipoanza ziara yake tarehe 3 Mei 2023.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.