Na Mashaka Mgeta, MOROGORO
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amewaasa wakulima kutumia fursa za mikopo rahisi ya zana za kilimo, ili kuchangia jitihada za Serikali za uboreshaji wa sekta hiyo.
Mhe Balozi Dkt Batilda, akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Mhe Ayubu Sebabile, ameyasema hayo leo Agosti 3, 2025, alipotembelea mabanda na vipando kadhaa kwenye Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro.
Amesema, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeboresha mazingira za kilimo, mifugo na uvuvi, kiasi cha kuzifanya kuwa rafiki kwa wadau hususani wakulima, kunufaika kupitia fursa kama vile mikopo hiyo yenye masharti nafuu.
Mhe Balozi Dkt Batilda, aliyasema hayo baada ya kukabidhi mkopo wa mashine ya kuchakata mpunga na trekta kwa wakulima wawili, Edwin Lipinga wa Kilosa na mwingine aliyejulikana kwa jina la Nola wa Kilombero.
Wakati Lipinga alikabidhiwa mashine ya kuchakata mpunga yenye thamani ya Shilingi milioni 56, Nola alikopeshwa trekta lenye ya Shilingi milioni 75 lililopokelewa kwa niaba yake na Peter Libana.
Mikopo hiyo imetolewa na kampuni ya Agricom kupitia Taasisi ya Mikopo ya Zana za Kilimo (PASS)
PASS iliyozinduliwa Julai 24, 2021 jijini Dodoma, inajishughulisha na utoaji mikopo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi pasipo dhamana.
Mkulima Libanga amesema anatarajia kuutumia mkopo huo kukuza ulizashaji wa mpunga atakaouchakata kuwa mchele, na hivyo kuuongezea thamani kwenye mauzo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PASS, Killo Lusewa, amewaalika wakulima kupata mikopo hiyo itakayowawezesha kukuza mitaji na kuinua hali hali ya maisha yao.
Mhe Balozi Dkt Batilda, amewawakilisha Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro kutembelea mabanda na vipando kwenye maonesho hayo.
Mhe Balozi Dkt Batilda alitembelea Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (MVIWATA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), kampuni ya Agricom, Bodi ya Pamba na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI).
Pia Mhe Balozi Dkt Batilda alizitembelea Halmashauri za Wilaya za Ulanga (Morogoro), Kibiti (Pwani), Kigamboni (Dar es Salaam), Muheza na Lushoto (Tanga).
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.