Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
WAHENGA walinena, ‘mgeni njoo mwenyeji apone’. Ndivyo ilivyo mkoani Tanga, baada ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu, kuhitimisha ziara yake ya siku saba mkoani humu.
Mhe Rais Dkt Samia, aliwasili Tanga Februari 23 na kufanya ziara kwenye halmashauri 11 za mkoani humo ambapo alikagua, kuweka jiwe na msingi na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo. Ziara hiyo ilifikia ukomo wake Machi Mosi, 2025.
Akihutubia maelfu ya wakazi wa Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani, Mhe Rais Dkt Samia, pamoja na mambo mengine, anaelezea nia yake ya kuurejesha mkoa huo kuwa ‘kitovu’ cha viwanda nchini.
Tanga yenye historia ya awali ya kuwa na viwanda kabla, wakati na baada ya uhuru, ilishuhudia kutoweka kwa sekta hiyo.
Mkazi wa Nguvumali, Mwanaidi Kihiyo, anasema ndoto ya Mhe Rais Dkt Samia, imeibua tumaini jipya kwa wakazi wa Tanga, wanaoamini kuwa kuwepo kwa viwanda kuchachochea ukujai uchumi, ajira na ustawi wa watu.
Mwanaidi akiwa na Bosco, wote wakifanya kazi kwenye moja ya viwanda vilivyopo Tanga, wanaelezea kushuhudia watu wengi hususani vijana, kuingia jijini humo kutafuta ajira viwandani.
“Sisi tunaofanya kazi viwandani na kumudu mahitaji yetu, tunajua maana halisi ya ndoto ya Mhe Rais Dkt Samia kuirejesha Tanga kuwa ya viwanda,’’ anasema Bosco Zakayo, Tunduma mkoani Songwe.
Anasema amefika Tanga takribani miaka miwili iliyopita na kupata ajira ya mkataba inayomfanya amudu maisha na mahitaji ya familia yake.
Hoja za wawili hao, zinafanana na maoni ya wafanyakazi wengi viwandani jijini Tanga, wakiasi hatua tofauti za mafanikio na maendeleo waliyonayo.
Meneja wa kiwanda kimoja ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema, idadi ya wanaofika kwenye maeneo ya viwanda ni kubwa ikilinganishwa na mahitaji, na wengi wao hurejeshwa kutokana na nafasi chache zilizopo.
Pia Meneja huyo anasema, baadhi ya viwanda husimamisha uzalishaji kutokana na athari za mazingira na hali ya hewa, hali inayowafanya wafanyakazi wengi kurejeshwa nyumbani.
“Sasa tunaiombea ndoto hii ya Mhe Rais Dk Samia itimie…ni dhahiri kwamba anakwenda kubaki kwenye historia ya mamilioni ya Watanzania,” amesema Meneja huyo.
Katika hotuba yake, Mhe Rais Dkt Samia, alisema anatamani kuirudisha Tanga ya viwanda kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.
Amesema hatua hiyo itaifungua zaidi Tanga kiuchumi kutokana na fursa za kiuchumi, biashara na kijamii ikiwemo utalii.
Mhe Rais Dkt Samia aliyasema hayo Februari 28, 2025 alipohutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa Mkwakwani jijini Tanga.
“Ninatamani kuirudisha Tanga ya viwanda kama ilivyo huko nyuma. Hili ndio tamanio langu kubwa,” amesema na kuongeza…
“Na mnapozunguka Tanga, mtaweza kuona hatua zimeanza kuchukuliwa. Kuna viwanda aidha vinafanyiwa utanuzi, au kuna maeneo majengo yanakuja. Ahadi yangu kwenu ni kuregeza masharti na kufanya masharti yawe mazuri zaidi ili waweke waweze kuja kwa wingi zaidi.”
Aidha, Mhe Rais Dkt Samia, amesema eneo jingine la kipaumbele katika kuchechemua uchumi wa Tanga ni kupitia ukuzaji wa sekta ya utalii hasa wa fukwe, historia na utamaduni.
Mhe Rais Dkt Samia amesema wakazi wa Tanga wanapaswa kuzichangamkia fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo bandarini na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Amesema, kutokana na kutoa kipaumbele kwa ukuzaji wa utalii, wananchi wanapaswa kujifunza taaluma zinazohusiana na sekta hiyo kama vile uongozaji wa utalii na utoaji huduma kwenye hoteli.
Mhe Rais Dkt Samia amesema uboreshwaji wa bandari ya Tanga uliogharimu Shilingi bilioni 429.1 umeanza kupunguza tatizo la ajira kwa vijana mkoani na Tanga na kutoka maeneo mengine ya nchi.
Amesema, Serikali ina mpango wa kuifanya bandari ya Tanga kuwa maalumu kwa ajili ya usafirishaji wa mazao kilimo na hivyo kuongeza shughuli zenye kutoa ajira kwa Watanzania.
Awali, Mbunge wa Tanga, Mhe Ummy Mwalimu, alisema hatua ya Serikali kufufua viwanda kutachangia kuongeza vipato vya wananchi walio wengi.
"Tanga ya miaka ya 80 ilikuwa ya viwanda na ilikuwa inashika nafasi ya pili ikiongozwa na Dar es Salaam, Mh. Rais, tunaomba utufufulie viwanda kwa manufaa ya wananchi wetu, vijana wapate ajira ili waendeshe maisha yao," alisema Mhe Ummy aliyewahi kuwa Waziri wa Afya.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.