Na Mashaka Mgetra, OMM TANGA
LICHA ya kuwepo dalili na ishara za wazi kwa Watanzania wengi kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali, wafanyabiashara mkoani wa Tanga, wameitumia hotuba ya Rais wa Kenya, Mhe William Ruto, kuthibitisha uongozi bora wa Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi wa nchi.
Mhe Rais Ruto, amekaririwa Ijumaa ya Novemba 29, 2024 akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha, akisema tofauti na nchi yake ambayo awali ilikuwa nafasi ya juu kwa mauzo ya bidhaa na huduma kwenye jumuiya hiyo, hivi sasa Tanzania ndio inayoongoza.
Mhe Rais Ruto amekaririwa akisema, ‘’ninaipongeza Tanzania kwa kuipiku Kenya kwa bidhaa na huduma tunazouza na kununua ndani ya Afrika Mashariki. Kenya ilikuwa nchi inayoongoza kwa bidhaa na huduma tunazouza na kununua kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki.’’
Mathalani, takwimu za kufikia Juni 2024 zinaonesha kuwa , Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Shilingi ya Kenya bilioni 540 kwa Uganda, hatua iliyoiwezesha kuchangia asilimia 42.56 na kuifanya (Tanzania) kuongoza kuingiza bidhaa nyingi zaidi Uganda ikifuatiwa na Kenya na Afrika Kusini.
Jana, kwenye viwanja vya Gulio la Tangamano ambapo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian amezindua ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA), Omar Mfumia, ‘akafungua pazia’ la kuunga mkono jitihada za kukuza uchumi za Mhe Rais Dk Samia, kiasi cha kuwavutia viongozi wa mataifa mengine akiwemo Mhe Rais Ruto.
‘’Nimealikwa hapa mbele niseme neno, lakini ninaomba Mhe RC (Mkuu wa Mkoa) uruhusu ili muongoza shughuli aliyepo kwenye vyombo vya sauti, atuwekee sehemu ya hotuba ya Mhe Rais Ruto wa Kenya, inayoelezea ukweli kuhusu ukuaji wa biashara, uchumi na huduma unaosimamiwa na Mhe Rais Dk Samia,’’akasema.
Ndipo sauti ya Mhe Rais Ruto iliposikika kama inavyoonekana pia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, akielezea namna Tanzania inavyoipiku Kenya katika nyanja za bidhaa na huduma kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Naye Mwenyekiti wa Soko la Tangamano, Yasin Chikirwa, akasema uongozi wake unaoendelea kutekeleza programu ya uboreshaji wa soko hilo, hautamvumilia mfanyabiashara ndogondogo asiyekuwa na kitambulisho.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema anasema kufanikiwa kwa hafla ya uzinduzi na ugawaji vitambulisho hivyo, kunadhihirisha namna Mhe Rais Dk Samia anavyotekeleza ahadi zake kwa vitendo, ikiwemo kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wafanyabiashara ndogondogo.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amesema kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tanga ina jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 60,253, kati yao, wanaume ni 37,137 na wanawake 23,116 na kwamba, miongoni mwa hao, 2,306 wametambuliwa, kusajiliwa na kati yao, wanawake ni 1,448 na wanaume 858.
Mhe Balozi Dk Batilda amesema mkoa huo umepokea vitambulisho 1,151 vilivyotolewa kwa walenga ili iwe chachu kwa wengine ambao bado hawajalipia Shilingi 20,000 kupitia control namba inayotolewa na mfumo wa GePG.
Aidha, amesema vitambulisho hivyo vitawawezesha wafanyabiashara ndogondogo kupata fursa ya mikopo katika benki ya NMB ambapo Serikali, kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetenga Shilingi bilioni 18.5 zitakazokopeshwa kwa wafanyabiashara hao kwa masharti nafuu na riba asilimia saba.
Mhe Balozi Dk Batilda amesema mpango wa kuwanufaisha wafanyabiashara ndogondogo unaotekelezwa na Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ni muitikio wa dhana ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa, ‘’maendeleo hayana budi yawe yana uhusiano na maisha ya watu na hakuna budi kuyapima yamefanya nini kwa watu.”
Uzinduzi wa kitaifa wa mpango huu ulifanyika jijini Arusha Oktoba 17, 2024 na Mhe Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Mhe Dk Dorothy Gwajima.
Mhe Mkuu wa Mkoa amesema, Tanga inaendeleza juhudi katika fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wake, na kuwezesha mazingira mazuri na hivyo, amewahimiza wafanyabiashara ndogondogo kuchangamkia fursa ya kupata vitambulisho hivyo vya kidijitali na kuinua uchumi wao.
Mhe Balozi Dk Batilda, amewaagiza wataalamu wanaowatambua na kuwasajili wafanyabiashara ndogondogo, kuzingatia utaalamu wao katika kulitambua kundi hilo ambalo Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, anawapa kipaumbele na kuwawezesha kushiriki katika kuinua uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.