Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
NDOTO ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuirejesha Tanga ya viwanda, inaendelea ‘kukuna vichwa’ vya viongozi na wakazi wa mkoa huo, ili kuifanikisha kwa maslahi mapana ya nchi na watu wake.
Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kimekutana Machi 6, 2025 chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, kikitawaliwa na hoja kadhaa, miongoni mwa hizo ni namna ya kuifikia ndoto ya Mhe Rais Dkt Samia kuhusu ‘Tanga ya Viwanda’.
Akizungumza na wakazi wa Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini humo Februari 28, 2025, Mhe Rais Dkt Samia, pamoja na mambo mengine, akasema, ndoto yake ni kuifanya Tanga irejee kuwa eneo huru la viwanda.
Ukuzaji viwanda linaibuka kwenye kikao hicho kutokana na kuwa sehemu ya Mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 kwa Fungu 086 la Mkoa wa Tanga yaliyowasilishwa kwenye RCC hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe Albert Msando, akasema, wakati Tanga ikirejeshwa kuwa ya viwanda, ipo haja ya kuwekeza katika uzalishaji wa malighafi za viwandani, ili kuwepo umiliki wa jumla wa umma katika uendeshaji wa sekta hiyo.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili, Handeni imepata viwanda vinne vya madini aina ya graphites vikiwemo vya kampuni ya In and Out inayozalisha tani 150 na viwili vya mfanyabiashara Godmwanga, kimoja kikizalisha tani 200 na kuingiza mapato ya Shilingi bilioni 60.
Mhe Msando amesema kiwanda kingine cha mfanyabiashara huyo kina uwezo wa kuzalisha kati ya tani 800 hadi 1,000 na kwamba bei katika soko la kimataifa kwa tani moja ni kati ya Dola za Marekani 400 hadi 1,000.
Akitumia takwimu hizo na uhalisia wilayani kwake, Mhe Msando akasema, kuwepo kwa viwanda vya kuongeza thamani, kutakuwa na maana zaidi na kumfurahisha Mhe Rais Dkt Samia, kama malighafi zitatoka kwa wakazi wa mkoa huo.
Mfano, Mhe Msando akasema bei ya mita za ujazo tani moja za madini aina ya Dolmites inayozalishwa na kusafirishwa ikiwa ghafi wilayani, kwenye soko la kimataifa inauzwa kati ya Shilingi milioni 18 na milioni 20.
Pia Mhe Msando akasema, hali hiyo inawiana na matumizi ya miundombinu mingine kama bandari na barabara, ambayo kama itahusisha bidhaa za ndani, mafanikio yake yatawagusa Watanzania walio wengi.
Mbunge wa Tanga Mjini, Mhe Ummy Mwalimu akasema, miongoni mwa malighafi zinazopaswa kutiliwa mkazo katika mipango ya kiuchumi mkoani humo ni mazao ya mifugo, kilimo na uvuvi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni, Mhe Mussa Mkombati, alisema ipo haja ya kutilia mkazo uwekezaji kwenye kiwanda cha kuzalisha mbegu bora za mazao ya kilimo, ili kukuza uzalishaji wenye tija na mazao bora kwa soko la ushindani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Mhe Akida Bahorora, amepongeza jitihada za Mhe Rais Dkt Samia kugawa boti kwa wavuvi.
Hata hivyo, ametahadharisha kwamba ipo haja ya kufuatilia matumizi yake, ili kudhibiti matumizi yaliyo kinyume cha malengo yake.
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Abdulrahman Shiloow, amesema ipo haja kwa uongozi wa mkoa wa Tanga, kuingilia kati na kuzisaidia halmashauri zinazodai madeni sugu kwa taasisi mbalimbali na wafanyabiashara, ili fedha hizo ziwezeshe kufanikisha mipango ya maendeleo na ustawi wa watu.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.