Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
UTEKELEZAJI wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF)-awamu ya tatu mkoani Tanga, umewaridhisha wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria waliopo kwenye ziara ya siku mbili mkoani humo.
Taarifa ya TASAF iliyosomwa na Katibu Tawala Mkoa (RAS), Pili Mnyema, imeeleza takribani Shilingi bilioni 15 zimetolewa na Serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa uhawilishaji kwa walengwa 68,906.
Mnyema alisema, kupitia utekelezaji wa miradi ya ajira za muda (PWP), Tanga imeibua miradi 750 kati ya 825 (sawa na asilimia 91) ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa TASAF.
Kwa mujibu wa Mnyema, miradi hiyo ilihusu ukarabati wa barabara za vumbi, vivuko vya waenda kwa miguu, bwawa na banio la umwagiliaji, vyanzo vya maji, miti ya mbao na upandaji miti ya matunda.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe Dkt Joseph Mhagama, amesema ufanisi wa miradi ya TASAF mkoani Tanga ni matokeo ya utashi wa kisiasa wa Mhe Rais Dk Samia, na usimamizi shirikishi wa viongozi mkoani humo.
Amesema mnyororo huo wa uongozi chini ya Mhe Rais Dkt Samia, unadhihirisha uwepo wa viongozi bora nchini na ambao, kimsingi, wanapaswa kutetewa na kulindwa wakati wote.
Mhe Dkt Mhagama, alitoa mfano wa viongozi hao kuwa ni Mkuu wa Mkoa, Mhe Dkt Batilda Burian, Katibu Tawala Mkoa, Pili Mnyema na wabunge wa majimbo na kuteuliwa wa mkoa huo, akiwemo Mhe Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo na mjumbe wa kamati hiyo.
Mhe Balozi Dkt Batilda alisema, Pamoja na TASAF, Tanga imepokea takribani Shilingi trilioni 3.1 kwa ajili ya miradi ya kisekta kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe Rais Dkt Samia.
Amesema, fedha hizo zimetumika kwa miradi ya maendeleo na ustawi wa jamii, pamoja na majengo ya utawala kwa halmashauri zikiwemo Bumbuli na Handeni Mji zilizozinduliwa na Mhe Rais Dkt Samia hivi karibuni.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.