Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
MOJA ya vigezo vinavyoitambulisha nchi kuwa na kiwango cha juu cha demokrasia ya kweli, ni mfumo wa Uchaguzi Mkuu ulio huru, wazi na haki, unaotoa fursa pana ya ushiriki wa wadau katika hatua zote za mchakato wake.
Ndivyo inavyodhihirika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 ambapo hivi sasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye mikoa ya Tanga na Pwani.
Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele, anafungua mafunzo ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Tanga leo Februari 2, 2025, yanayowashirikisha Mratibu wa Uandikishaji Mkoa, Maafisa Uandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri.
Anasema, Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakidhi vigezo ambavyo (kwa mujibu wa misingi ya uchaguzi huru na haki) vitaing’arisha nchi kimataifa, ikiwemo kuwaruhusu waangalizi wa nje na ndani ya nchi kushiriki kwa upana zaidi.
Jaji Mwambegele anasema taasisi 42 za waangalizi wa ndani na nje ya nchi, zimethibitishwa kushiriki uangalizi wa uchaguzi huo, ambapo kati ya hizo, tisa ni za kimataifa na 33 za kitanzania.
Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, taasisi hizo zinapaswa kupewa ushirikiano katika ngazi ili zitimize wajibu na majukumu yao ipasavyo, yatakayoudhihirishia ulimwengu ukweli kuhusu ubora wa uchaguzi wa Tanzania utavyofanyika kwa misingi ya uhuru, haki, amani na uwazi.
Mbali na waangalizi hao, Jaji Mwambegele amesema fursa nyingine inayodhihirisha utayari wa Serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kufanya uchaguzi huru na haki ni ushiriki wa taasisi za kiraia 157 zitakazotoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi huo wenye kauli mbiu inayosema, ‘’Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora’.
UTUNZAJI VIFAA VYA UANDIKISHAJI
Jaji Mwambegele amewaagiza maafisa wanaohusika na uchaguzi kuvitunza vifaa vya uboreshaji na uandikishaji wapiga kura, kwa vile vimegharimu fedha nyingi na vinahitajika kwenye maeneo mengine.
Amesema, kutokuwa makini katika utunzani wa vifaa hivyo, kutaathiri mwenendo wa uboreshaji na uandikishaji wapiga kura kwenye mikoa, wilaya na halmashauri ambazo hazijafikiwa na huduma hiyo.
INEC inatarajia kuandikisha wapiga kura 244,805 mkoani Tanga ikiwa ni sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 1,304,235 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, na hivyo kufanya idadi yake kufikia 1,549,040.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.