Na Mashaka Mgeta, OMM TANGA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeelezea kustaajabishwa na kasi kubwa ya maendeleo kwenye bandari ya Tanga, iliyoboreshwa kwa gharama za Serikali ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe Selemani Kakoso, amesema aliposhiriki ziara ya Mhe Rais Dkt Samia bandarini hapo Machi Mosi, 2025, alishuhudia ‘mabadiliko makubwa’, ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa Mhe Kakoso, Kamati hiyo ilifanya ziara bandarini hapo mwaka 2023 na kubaini umuhimu wa kuwepo maboresho, ili ichangie ufanisi katika mpango wa kuifanya Tanga kuwa Mkoa wa ki-mkakati katika masuala ya uchumi na biashara.
Mhe Kakoso anasema katika kipindi hicho, Kamati yake ilibaini ucheleweshwaji wa malipo kwa maboresho ya bandari hiyo, hivyo kuishauri Serikali itoe fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili hiyo.
Hata hivyo, Mhe Kakoso, licha ya kutotaja kiasi cha fedha walichotarajia, anasema Shilingi bilioni 429.1 zilizotolewa kwa wakati mmoja zilikuwa nyingi, na hivyo kudhihirisha utashi wa Mhe Rais Dkt Samia katika kufanikisha maboresho ya bandari hiyo.
“Nilitembelea bandari hiyo na kamati hii mwaka 2023, tukaikuta katika hali duni na miundombinu isiyokidhi ufanisi na ushindani kwenye soko, lakini fedha nyingi zilizotolewa na Mhe Rais Dkt Samia zimefanya maboresho na kuleta maendeleo makubwa sana,” amesema.
Amesema, Serikali inapaswa kushughulikia miundombinu wezeshi itakayochochea ufanisi wa huduma za bandarini ikiwemo reli na ujenzi wa barabara ya Handeni - Kibirashi - Kiteto – Nchemba - Singida yenye urefu wa kilomita 460 na ile ya Tanga - Pangani - Saadan – Makurunge (kilomita .
Hata hivyo, akiwa katika ziara yake mkoani humu, Mhe Rais Dkt Samia, aliiagiza Wizara ya Miundombinu kushirikiana na wadau wengine ikiwemo sekta binafasi ili kugharamia ujenzi wa barabara ya Handeni - Kibirashi - Kiteto - Nchemba – Singida yenye kilomita 460.
UMUHIMU WA ZIARA ZA WABUNGE
Mhe Kakoso anasema ziara zinazofanywa na Kamati za Bunge zina manufaa makubwa, ikiwemo ‘kuisukuma’ Serikali kukamilisha miradi hasa inayokwamishwa kutokana na ukosefu wa fedha.
Amesema ziara hizo zinatajwa kwenye Kanuni za Bunge na hivyo kuzihalalisha hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye bajeti ya mwaka mpya wa fedha 2025/2026.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.