Na Mashaka Mgeta, DAR ES SALAAM
ILE kauli mbiu ya ‘Tanga Lango Kuu la Uchumi Afrika Mashariki’ inazidi kutanua wigo wa maendeleo ya wakazi wa mkoa huo, kutokana na hatua mbalimbali ikiwemo ushiriki wa wafanyabiashara na wajasiriamali wake kwenye maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Wafabiashara na wajasiriamali hao wanaofikia 17, wanasema ubunifu, ushirikishaji na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe Balozi Batilda Burian, kuwagharamia kushiriki maonesho hayo yenye hadhi kubwa ya kufungua na kuongeza fursa za kiuchumi, haijawahi kutokea kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita.
Baada ya kuwasili mkoani Tanga Machi 13, 2024 kufuatia kuhamishiwa kutokea mkoani Tabora Machi 9, 2024, Mhe Balozi Dk Batilda akasema miongoni mwa njia za kuipa maana kubwa kauli mbiu ya ‘’Tanga Lango Kuu la Biashara Afrika Mashariki’’ ni pamoja na kuwapa fursa wafanyabiashara na wajasiriamali mkoani humu, ni kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wenyeji kushiriki maonesho hayo.
Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Tanga, Pili Mnyema, amewatembelea wafanyabiashara na wajasiriamali hao jana Julai 7, 2024, akazungumza nao na kuwahakikishia nia ya Serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu, kukuza na kuwajengea uwezo zaidi wa kumudu ushindani kwenye soko.
Siri Sadik maarufu kama Binti Sadi, mjasiriamali wa Pangani anayetengeneza bidhaa za asili kwa matumizi mbalimbali, zikitokana na malighafi zinazopatikana mkoani Tanga, anasema ingawa hii ni mara ya 12 kushiriki maonesho hayo, lakini mwaka huu, asingeshiriki kutokana na uwezo mdogo wa kifedha, hadi alipojulishwa kuhusu mwaliko wa Mhe Balozi Batilda kwao.
‘’Mwaka huu sikuwa na wazo la kuja Sabasaba kutokana na hali ya kifedha kutokuwa nzuri, lakini Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga, na kupitia jitihada za Mhe Balozi Batilda, nimeweza kushiriki, tena kwa namna ambayo haijawahi kutokea, kwa maana tofauti na wakati mwingine, safari hii tunatambulika rasmi kwenye banda la mkoa wa Tanga,’’ anasema.
Mjasiriamali anayesifika zaidi kwa biashara ya unga bora wa mwani, Hajra Ali, anasema ushiriki wake wa mara kwanza kwenye maonesho hayo, umemfungua ufahamu zaidi wa kutambua namna tofauti za uzalishaji, usindikaji na kutafuta masoko, hivyo kumuongezea ujuzi, mbinu na stadi kwenye biashara zake.
‘’Ingawa kwa upande wa mauzo naona yapo chini kuliko nilivyotarajia, lakini nimepata mbinu, stadi na ujuzi mkubwa sana wa namna ya kushiriki na kukuza biashara zangu,’’anasema.
Mjasiriamali Grace Anania anasema, kabla ya kujiunga na kampuni ya Enika Collections inayotengeneza bidhaa zinazotumia zaidi nyuzi za katani, alikuwa hajaelewa manufaa ya ujasiriamali huo, lakini sasa anafikiria kukua zaidi kupitia uzoefu na kujifunza kutoka kwa washiriki wengine wa maonesho hayo.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.