Na Mashaka Mgeta, OMM-TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Batilda Burian, amewakabidhi Wakuu wa Wilaya tatu na Afisa Mipango wa mkoa huo, jumla ya magari manne yenye thamani ya Shilingi 833,854,796 kwa ajili ya matumizi ya ofisi.
Wakuu wa Wilaya waliokabidhiwa magari hayo aina ya Prado yenye namba STN 2880, STN 2879, STN 2881 na wilaya zao kwenye mabano ni Mhe Hashim Mgandilwa (Kilindi), Mhe William Mwakilema (Korogwe) na Mhe Mussa Kilakala (Pangani).
Pia Afisa Mipango wa Mkoa, Amina Said, alikabidhiwa gari aina ya Landcruser Hard Top yenye namba STN 2888 lenye thamani ya Shilingi milioni 150, wakati magari ya Wakuu wa Wilaya yamegharimu Shilingi 227,951,598.79 kila moja.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amewakabidhi viongozi hao magari hayo, na kuelekeza yatumike katika kusimamia, kufuatilia na kufanikisha miradi ya maendeleo na mipango ya ulinzi na usalama wa watu na mali zao.
Kwa mujibu wa Mhe Balozi Dk Batilda, Serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, imepanga kutumia Shilingi bilioni 1.1 kwa ununuzi wa magari mengine mkoani Tanga kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
‘’Hili ni deni kubwa tunalopaswa kulilipa kwa Mhe Rais Dk Samia, kipenzi cha Watanzania kwa kuhakikisha magari haya yanatunzwa na kufanya kazi zilizokusudiwa,’’ amesema.
Amesema magari hayo yawe chachu ya utendaji kazi ikiwemo kufanikisha ziara za Wakuu wa Wilaya kutembelea wananchi, kusikiliza na kutatua kero zao.
Katibu wa Mkoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Seleman Sankwa, amesema magari hayo ni miongoni mwa vilelezo vya mafanikio ya Mhe Rais Dk Samia, ambaye kwa msimamo walio ndani na nje ya chama hicho, malipo yake ni kumchagua katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Amesema, Wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Idara ya Mipango waliokabidhiwa magari hayo, wanapaswa kuendeleza uadilifu na kuepuka matumizi yanayoweza kuibua taswira hasi kwa jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wakuu wa Wilaya hao wameahidi kuyatunza na kuyatumia ili kufikia matarajio ya Mhe Rais Dk Samia, kuongeza mapato ya ndani na kuwafikia, kuwasikiliza na kutatua kero wananchi.
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.