Na Mashaka Mgeta, KOROGWE
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Dk Ashatu Kijaji, amewahimiza wazazi na walezi, kutilia mkazo malezi bora yanayowajenga watoto kimaadili, ili kuwa na kizazi chenye tija kwa maendeleo endelevu wan chi.
Mhe Dk Kijaji amesema, fedha nyingi zinazotolewa na Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa miundombinu na huduma katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, haitakuwa na maana kama watoto watakua katika mmomonyoko wa maadili, na hivyo kushindwa kuwa na stadi na maarifa yanayowastahili.
Mhe Dk Kijaji ametoa rai hiyo kwa nyakati tofauti na leo Januari 9,2025, alipotembelea shule za sekondari za Lunguza na Rashid Shangazi (Lushoto), Nyerere, Semkiwa, Makorola na Foroforo wilayani Korogwe.
Amesema sekta ya elimu ni miongoni mwa maeneo ya vipaumbele kwa Rais Dk Samia, hivyo kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, ili kuwepo na elimu bora kwa kila mtoto wa kitanzania.
Hata hivyo, amesema nia njema hiyo ya Mhe Rais Dk Samia, inapaswa kuendana na utayari wa wazazi na walezi, kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema, na kuepuka kuwaita majina yasiyofaa kama vile ‘Watoto wa Siku Hizi’.
‘’Hawa ni watoto wetu, mnapowaita ‘Watoto wa Siku Hizi’ huyo ‘Siku Hizi’ ni nani,’’anahoji Mh Dk Kijaji.
Pia, Mhe Dk Kijaji amewaasa watoto waliopo mashuleni, kusoma kwa bidii na kujiepusha na vitendo vinavyochangia kuwaathiri kwa namna tofauti na hatimaye kuwakatisha masomo.
Amesema kupata na kuhitimu elimu bora kunachangia kuwajengea uwezo na maarifa watoto kuwa viongozi bora wa baadaye, akitoa mfano wa Mhe Rais Dk Samia.
‘’Mkiwa wasikivu na watiifu kwa wazazi na walezi wenu, mkiwasikiliza walimu na kufuata na kuyashika wanayowafundisha, mtapata manufaa bora zaidi kwa baadaye,’’ ameasa.
Akiwa wilayani Korogwe leo, Mhe Dk Kijaji ametembelea, kukagua na kuweka mawe wa msingi kwenye miradi yenye thamani ya jumla ya Shilingi 1,820,880,029.
Miradi hiyo na thamani ya kila mmoja kwenye mabano ni madarasa matano na matundu nane ya vyoo katika Shule ya Sekondari Nyerere (139,400,000), madarasa matatu na matundu nane ya vyoo katika Shule ya Sekondari Semkiwa (89,400,000).
Mingine ni shule mpya ya sekondari Makorola (584,280c,29), nyumba ya Afisa Ugani katika kata ya Magoma (40,000,000) na miundombinu ya madarasa, nyumba ya walimu, matundu ya vyoo na mabweni Shule ya Sekondari Foroforo (739,000,000).
Golf Area/Masiwani Road Tanga
Anuani ya posta: P.O.Box 5095 Tanga
Simu: 027 2642421
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ras.tanga@tamisemi.go.tz
Haki miliki ©2017 Katibu Tawala Mkoa wa Tanga . Haki zote zimehifadhiwa.